Saturday, July 7, 2012

UNICEF yasema watoto wananyanyaswa kaskazini mwa Mali

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto, UNICEF, limesema kuwa mabomu ya kutegwa ardhini yaliyozikwa na makundi ya Kiislamu kuzunguka miji ya Gao na Timbuktu kaskazini mwa Mali, ni kitisho kikubwa kwa watoto.
Shirika hilo limesema kuwa tayari mabomu hayo yamekwishauwa watoto wawili, na wengine wapatao 8 wamekwishajeruhiwa na mabomu hayo na miripuko ya aina nyingine.

UNICEF pia imesema kuwa watoto katika maeneo yanayoshikiliwa na makundi hayo wananyanyaswa kijinsia, na kwamba wavulana wapatao 175 wameandikishwa kama wapiganaji, na shule zilifungwa tangu Machi.


Mwakilishi wa UNICEF nchini Mali, Theophane Nikyema, amesema kuwa hali hiyo inazua wasiwasi, ikizingatiwa kuwa hayo ni sehemu ndogo tu ya masaibu yanayowasibu watoto katika maeneo ambayo ni vigumu kufikiwa na wafanyakazi wa mashirika ya kibinadamu.

 UNICEF imeibainisha hali hiyo siku moja kabla ya mkutano maalum juu ya Mali, ambao utafanyika kesho nchini Burkina Faso. 

No comments:

Post a Comment