Friday, October 12, 2012

AFISA UHAMIAJI MWANZA ANUSURIKA KUUAWA NA POLISI MWANZA

AFISA wa Uhamiaji ofisi ya Mkoa wa Mwanza Albert Buchafwe amenusurika kuuawa kwa risasi baada ya kushambuliwa na Mkuu Msaidizi wa Kituo cha Polisi Nyakato, Abubakar Zebo kwa madai kuwa walikuwa wakishambulia jambazi.
 
Kamanda Liberatus Barlow.
Tukio hilo ambalo limethibitishwa na kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow linadaiwa kutokea majira ya saa 4: 13 usiku wakati afisa huyo wa uhamiaji  akiwa njiani kuelekea nyumbani kwake ambapo alikutana na gari dogo aina ya Suzuki lililomuashia taa likimuashiria kusimama.
 
Akielezea mkasa kamili Buchafwe alisema kwamba baada ya kuwashiwa alipochunguza kwa makini gari hilo aliweza kulibaini kuwa ni lile linalotumika na afisa huyo wa Polisi, hivyo alisimama na kujitambulisha kwake akiwa ndani ya gari lakini aliamuriwa kuzima taa za gari lake na kutoka ndani yake.
 
“Nilitii nikazima taa, lakini nilisita kutoka katika gari langu, nilijitambulisha kwamba mimi ni afisa Uhamiaji na kumtaja jina afisa huyo, ambaye aliendelea kunilazimisha kushuka ndani ya gari huku nikiona akijiweka sawa ikiwa ni pamoja na kuandaa Bastora yake tayari kwa kushambulia,” alieleza.
 
Alisema wakati bado akijitambulisha alishuka askari aliyekuwa na sale katika gari hilo la afisa huyo wa polisi akiwa na silaha ya SGM hali ambayo ilimlazimu kugeuza gari haraka na kukimbia huku gari lake likishambuliwa nyuma kwa risasi.
 
“Gari langu limeshambuliwa kwa risasi zaidi ya tano, moja imetoboa upande wa mbele karibu na Tairi ya kulia, risasi tatu zimetoboa nyuma ya gari na moja ubavuni mwa gari upande wa nyuma, lakini sikuweza kupata madhara, hali ambayo ilinilazimu kukimbia hadi ofisini kwangu na kutoa taarifa kwa bosi wangu wa mkoa usiku huo,” alizidi kufafanua.
 
Buchafwe alisema amepatwa na mashaka na tukio hilo kutokana na asakri huyo aliyehusika kuwa na mahusiano ya karibu na mkewe ambaye wamekuwa na ugomvi naye pamoja na kesi ya kutalikiana mahakamani na kusema kwamba huenda lilikuwa la bahati mbaya.
 
“Nina kesi na mke wangu mahakamani, na afisia huyu wa polisi amekuwa na mahusiano ya karibu na mke wangu huyu ambaye tunashitakiana mahakamani, inanishangaza kwamba mtu ambaye ananifahamu licha ya kujitambulisha bado alikuwa akishilikilia msimamo wa kunitaka kushuka, nadhani hapa kuna jambo zaidi ya hali ilivyo,” alieleza.
 
Aidha akizungumzia tukio hilo kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza alikiri kuwapo kwake na kudai kwamba anayo hakika kwamba tukio hilo limetokea kwa bahati mbaya kwani jeshi lake lilipata taarifa za Kiinterejensia za kuwapo kwa majambazi wakidaiwa kutumia gari sawa na ambalo afisa huyo wa uhamiaji alikuwa nalo.
 
“Hili ni tukio la bahati mbaya, jeshi laetu lilipata taarifa za Kiinterejensia juu ya kuwapo kwa majambazi na kuamua kuweka mtego, sasa afisa huyu alifika muda na wakati ambao askari wetu walikuwa eneo hilo na kuingia katika mtego wetu, alikuja na gari ambalo ni sawa na lile ambalo tulielezwa kuwa lingetumika, lakini bahati nzuri mauaji hayakutokea,” alifafanua kamanda huyo.
 
Kamanda Barlow amedai kwamba kutokana na tukio hilo amepanga kukutana na afisa huyo wa uhamiaji na kuzungumza naye akiwa na askari wake kutafuta suluhu ya jambo hilo ambalo aliekeza kwamba yeye anaamini limetokana na bahati mbaya.

No comments:

Post a Comment