Rais Mohammed Mursi ameapa kwamba haki itatendeka kwa maafisa wa wakati wa mtangulizi wake, Hosni Mubarak, ikiwa ni siku moja baada ya uamuzi wake wa kumfukuza kazi mwendesha mashitaka mkuu wa serikali kuwakasirisha majaji nchini humo.
Jana Mursi alifungua upya mgogoro wake na majaji baada ya kumtimua kazi mwanasheria huyo, Abdel Maguid Mahmoud, kwa tuhuma za kuwasilisha ushahidi dhaifu mahakamani kwa watuhumiwa wa mashambulizi dhidi ya waandamanaji yaliyomng'oa madarakani Mubarak.
Mahmoud amekataa kuondoka kwenye wadhifa wake, na baadhi ya majaji wa ngazi za juu wanamuunga mkono. Akizungumza baada ya sala ya Ijumaa, mjini Alexandria, Mursi amesema kwamba kamwe serikali yake haitawaacha wale waliofanya uhalifu dhidi ya taifa na kulifisidi.
Mjini Cairo, mapigano yamezuka katika uwanja wa Tahrir kati ya wafuasi wa Mursi na wapinzani wake wakipigania udhibiti wa uwanja huo. Kiasi cha watu 10 wamejeruhiwa pale makundi hayo mawili yaliporushiana mawe. Haya ni machafuko mabaya kabisa tangu Mursi kuingia madarakani, miezi minne iliyopita.
Maandamano hayo yanafuatia kukataa kwa mwendesha mashitaka mkuu kuachia wadhifa wake, baada ya kuondolewa madarakani na Rais Mursi.
No comments:
Post a Comment