TAARIFA YA UCHUNGUZI WA KIFO CHA MWANDISHI WA HABARI WA CHANNEL TEN BW. DAUD MWANGOSI
1.0 UTANGULIZI
Mnamo tarehe 03 Septemba mwaka 2012, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi (MB) aliteua Kamati ya watu watano kufanya uchunguzi kuhusiana na kifo cha mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, marehemu Daud Mwangosi, kilichotokea tarehe 02 Septemba 2012, katika Kijiji cha Nyololo,Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa. Kituo cha kazi cha marehemu Daud Mwangosi kilikuwa mkoa wa Iringa ambapo pia alikuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Iringa (IPC).
Wajumbe wa Kamati hiyo ni:
Jaji (Mst.) Steven Ihema – Mwenyekiti
Bibi Pili Mtambalike – Mjumbe
Kanali (Dkt. Eng) Wema Wilson Wekwe – Mjumbe
Bwana Theophil Makunga – Mjumbe
Naibu Kamishna wa Polisi Issaya Juma. Mngulu – Katibu
Sekretarieti ya Kamati ni:
Bi. Edith T. Assenga – Wizara ya Mambo ya Ndani
Bwana Nasoro H. Msumi – Wizara ya Mambo ya Ndani
2.0 HADIDU ZA REJEA
Kamati ilipewa Hadidu za rejea zifuatazo:
- Uhalali wa mkusanyiko ulioitishwa na CHADEMA eneo la Nyololo,Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa tarehe 02 Septemba, 2012 na kuwepo kwa uvunjifu wa amani.
- Kama yalikuwepo makubaliano au maelekezo kuhusu mikutano ya hadhara au maandamano nchini katika kipindi cha Sensa.
-Mazingira yaliyosababisha Jeshi la Polisi kutumia nguvu iliyosababisha kifo cha Marehemu Daud Mwangosi na wengine kuumizwa, na uwiano wa nguvu hiyo na tukio.
-Madai ya kuwepo uhasama kati ya Jeshi la Polisi na Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa na chanzo cha uhasama huo. Aidha kuna madai ya kuwepo kwa orodha ya waandishi watatu (3) ambao Jeshi la Polisi limepanga kuwashughulikia.
-Uwepo wa Sheria, Kanuni au Taratibu zinazotoa uwezo kwa Jeshi la Polisi kuzuia mikusanyiko inayoitishwa na Vyama vya Siasa na Mamlaka ya Rufaa endapo vyama hivyo havitaridhika na amri hizo.
-Hali ya Mahusiano kati ya Jeshi la Polisi na Vyama vya Siasa nchini katika Utendaji kazi wao na Utii wa Sheria.
3.0 MUDA WA UCHUNGUZI
Kamati ilipewa muda wa siku 19 kuanzia tarehe 11 Septemba 2012 iwe imekamilisha uchunguzi na kuwasilisha Ripoti yake ifikapo tarehe 02 Oktoba 2012.