NAANZA kuandika simulizi hii kwa kumshukuru Mungu kwanza, kwa kuninusuru na mlipuko wa bomu uliotokea Jumamosi ya Juni 15, mwaka huu, katika mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wa kuhitimisha kampeni za udiwani wa katika kata nne za ndani ya Jiji la Arusha.
Kwa hakika kabisa, Jumamosi hiyo ya Juni 15, 2013, ‘imejenga mnara’ wa kumbukumbu mbaya ndani ya moyo wangu, na itanichukua muda mrefu kidogo kusahau tukio hilo la kutisha na kuhuzunisha sana.
Naikumbuka siku hiyo vizuri. Kwanza, tofauti na siku zote, siku hiyo niliamka saa nne asubuhi, badala ya muda wangu wa kawaida wa saa 12:30 au saa moja asubuhi. Hiyo ilitokana na kwamba jana yake, yaani Ijumaa ya Juni 14, nilikuwa katika safari ndefu ya kutoka Iringa hadi Arusha nikitumia usafiri wa umma.
Nilikuwa Iringa kwa siku tano kuhudhuria warsha ya Wahariri na Waandishi wa Habari Waandamizi kutoka mikoa yote nchini kuhusu ujangili, iliyokuwa imeandaliwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Kwa hiyo, kutokana na safari hiyo ndefu, mimi na waandishi wenzangu Musa Juma na Anthony Mayunga (Mwananchi), David Ruennyagira (Radio 5) na Eliya Mbonea (New Habari (2006) Ltd) tulifika Arusha mjini usiku wa manane, tukiwa na uchovu mwingi.
Baada ya kupumzika nyumbani na kupata chakula cha mchana, nilikwenda mjini Arusha nikiwa nimeambatana na wanangu wawili, Laureen (12) na Lantah-Sonia (4), na moja ya malengo yangu katika safari hiyo, ilikuwa ni kushuhudia uhitimishaji wa kampeni za uchaguzi kwa vyama vyote vilivyokuwa vinashiriki uchaguzi wa madiwani wa kata nne zilizokuwa zikigombewa.
Nilichagua kuanza na kata ya Kaloleni kutokana na kata hiyo, kwa sehemu kubwa, kuwa eneo la mji na pia vyama vya CHADEMA, CUF na CCM vyote vilikuwa vinahitimisha mikutano yao ya kampeni katika kata hiyo.
Kwanza nilianza na mkutano wa Chama cha Wananchi (CUF) uliokuwa unafanyika jirani na uwanja wa Sheikh Amri Abeid. Hata hivyo, mkutano huo haukuwa na watu wengi wala shamrashamra zozote, na hata mgombea wa chama hicho, Abbas Darwesh, alikuwa bado hajaanza kuzungumza.
Hali hiyo ya msisimko mdogo katika mkutano huo wa CUF, ilinifanya niamue kwenda kwenye mkutano wa CCM uliokuwa ukifanyika Ilboru, mkabala na ofisi za Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF), ambao mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye.
Mkutano ulikuwa na mahudhurio makubwa na shamrashamra nyingi. Nilisikiliza hotuba za viongozi na makada mbalimbali wa CCM hadi saa 10:45, nilipoamua kuondoka hapo na kwenda kwenye mkutano wa CHADEMA ambao walikuwa katika viwanja vya Soweto, umbali wa kama mita 500, kutoka eneo ambalo CCM walikuwa wakihitimisha kampeni zao.
Kabla ya kuingia ndani ya viwanja hivyo, nilitafuta sehemu salama ya kuegesha gari langu. Kutokana na umati wa watu nilioukuta katika viwanja hivyo, niliamua kuegesha gari hilo katika nyumba za AICC (Soweto Flats), umbali wa mita takriban 300 kutoka viwanja vya Soweto, nyumbani kwa mama mmoja ambaye ni rafiki wa familia yangu, na zaidi watoto wa mama huyo na wa kwangu wanasoma shule moja. Hapo ndipo lipowaacha pia watoto wangu wawili hao.
Nilifika eneo la mkutano, kwa kweli uwanja wa Soweto ulikuwa umejaa watu. Nilijaribu kupenya ndani ya umati huo wa watu hadi eneo la jukwaa kuu ili nipate fursa nzuri ya kuwasikiliza viongozi na makada wa chama hicho wakinadi sera zao.
Hali ilikuwa ya utulivu mkubwa katika mkutano huo, huku mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, akiwa jukwaani akiwanadi wagombea, na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, pamoja na viongozi wa ngazi ya wilaya na mkoa wakiwa jukwaa kuu.
Kutokana na wingi wa watu muda wote nilikuwa nyuma ya gari la matangazo ambalo pia hutumika kama jukwaa na viongozi walikuwa juu ya gari hilo.
Baada ya Lema kumaliza, alimkarabisha Mbowe na wakati anaanza kuhutubia, ilikuwa yapata saa 11:20 jioni. Nilimwomba mpiga picha wa mtaani anayefahamika kwa jina la ‘Photo me’ atumie kamera yangu ndogo kupiga picha za umati ule wa watu pamoja na Mbowe akiwa jukwaani.
Nilikaa kwa muda kidogo eneo hilo la nyuma ya gari la matangazo, baadaye nilipenya pembeni ya gari hilo la matangazo ili niweze kwenda mbele ya jukwaa, lakini nikakutana na kizingiti cha kuzuiwa na mmoja wa walinzi wa kike wa CHADEMA, maarufu kwa jina la Red Brigade.
Wakati mlinzi huyo ananizuia, baadhi ya viongozi wa CHADEMA, akiwamo Judith William, Katibu wa Baraza la Wanawake wa chama hicho (Bavicha), Kata ya Sokoni One, aliyepoteza maisha katika tukio hilo la bomu, waliingilia kati na kumtaka mlinzi wao huyo asinizuie kwa kuwa mimi ni Mwandishi wa habari.
Hatimaye mlinzi yule aliniruhusu nikaingia eneo la mbele ya jukwaa. Nilisalimiana na baadhi ya viongozi na makada wa chama hicho tunaofahamiana nao, akiwamo kada maarufu wa CHADEMA katika siasa za Arusha, Kalist Lazaro.
Aidha, eneo hilo la mbele kulikuwa kumekaliwa na viongozi wa ngazi za kata kutoka wilaya ya Arusha mjini, pamoja na watoto wadogo waliokuwa wamekaa chini, wapiga picha wa vituo mbalimbali vya televisheni na wapiga picha wa kujitegemea.
Freeman Mbowe, baada ya kukaribishwa na Lema, alihutubia mkutano huo hadi saa 11:45, alipohitimisha kampeni hizo kwa kumtaka Lema kutangaza utaratibu wa kuondoka eneo lile kwa maandamano kuelekea kata ya Elerai.
Nami nilichukua nafasi hiyo kuondoka mbele ya jukwaa kuu kwa nia ya kumfuata mpiga picha aliyekuwa na kamera yangu, kabla ya kuungana na diwani wa Levolosi, Ephata Nanyaro, aliyeshuka jukwaani na baada ya kusalimiana, tulianza kuondoka eneo hilo la mkutano.
Lakini wakati bado tunashangaa eneo hilo, ghafla kukatokea kishindo kikubwa kilichoambatana na sauti ya kuogofya. Watu walianza kukimbia ovyo kuelekea huku na kule, na katika purukushani hizo, nilijikuta nikipigwa kikumbo kilichonisukuma hadi mtaroni, na kupata maumivu makali ya goti.
Kulikuwa na taharuki kubwa. Nilipoinuka kutoka mtaroni, nilimuona diwani Nanyaro akiwazuia watu kwa kuwatuliza, akisema kuwa ni ‘tairi la gari limepasuka’, lakini wakati huo huo kupitia gari la matangazo la CHADEMA, nikasikia sauti kali ya mbunge Lema ikisema; tumeshambuliwa kwa bomu.
Nilijaribu kurudi mbele ya gari la matangazo. Nilipofika mahali pale, ilikuwa balaa tupu. Zaidi ya watu 15 walikuwa chini huku damu zikiwa zimewatapakaa na katika eneo zima hilo mithili ya wanyama waliochinjwa. Kulikuwa na watoto wadogo, wanawake na watu wazima.
Nilimtambua kwa haraka Mama Judith William aliyekuwa amelala chini, huku akiwa ametapakaa damu mwili mzima, hali ilikuwa inatisha. Kwa haraka, nilikumbuka muda mfupi tu uliopita tulikuwa tumesimama eneo moja, na eneo hilo hilo ndipo bomu limetupwa. Alikuwa ameuawa kinyama. Sikuamini macho yangu!
Kulikuwa na watoto wadogo wamelala chini wakiwa na maumivu makali, hii ilinitisha sana na kunitia huruma, na hasa nikikumbuka kuwa hata nami nilikuwa mzazi wa watoto wenye umri kama niliowaona pale chini.
Nilijaribu kutoa kamera nipate picha ya mahali pale, lakini muda huo huo Polisi walianza kurusha mabomu ya kutoa machozi, na nikaanza kusikia milio ya risasi. Ilikuwa ni tafrani ambayo sikuwahi kuishuhudia.
Bomu lilitua karibu yangu na kulipuka, nilikimbilia eneo la wazi na wakati huo viongozi na makada wa CHADEMA walikuwa wanajaribu kuwaokoa majeruhi kuwapakia katika magari na kuwakimbiza hospitali.
Wakati nakimbia kujiokoa na risasi za moto na mabomu ya machozi nilimwona Mwenyekiti Mbowe akiwa amembeba mmoja wa watoto waliojeruhiwa, akiwa ametapakaa damu na kumpakia kwenye gari. Nilikimbia bila kusimama hadi nilipoacha gari langu na muda wote mabomu machozi yaliendelea kurushwa.
Nilipofika kwenye gari niliona kwa mbali gari la polisi pia likiondoka kwa kasi eneo hilo, nami pia niliondoa gari hadi baa maarufu ya Arusha Night Park na kuliegesha hapo.
Muda huo nilijaribu kuwasilina na Mhariri Mkuu wa gazeti hili la Raia Mwema, Godfrey Dilunga, kumweleza hali iliyotokea, lakini simu zilikuwa haziendi, na hii ilikuja kubainika baadaye kuwa kwa muda ule wa tukio hilo, mitandao yote ya simu ilikuwa haifanyi kazi.
Nilitafakari sana juu ya hatua ya polisi kurusha mabomu wakati walipaswa kutoa msaada wa kuokoa watu na kuwawahisha hospitali, sikupata jibu hadi wakati naandika simulizi hii.
Baada ya kuegesha gari nilirudi kwa miguu hadi uwanja wa Soweto. Niliwakuta makada wachache wa CHADEMA waliokuwa wanajaribu kuzuia (kulinda) eneo la mlipuko, huku eneo hilo likiwa na mabaki ya nguo, viatu na damu iliyotapakaa.
Niliendelea na kazi zangu kama mwandishi wa habari, licha ya kuwa na kumbukumbu za kuuawa kwa watu niliosalimiana nao muda mfupi hapo uwanja wa mkutano. Muda mfupi baadaye, nilikwenda Hospitali ya Selian. Huko majeruhi walikuwa wamefurika, huku madakatari na wauguzi wakijitahidi kutoa huduma ya kwanza na nje ya viwanja vya hospitali kulikuwa na umati mkubwa wa watu.
Kila moja alikuwa na ushuhuda wake, wengine walidai kumwona aliyerusha bomu likiwa katika mfuko mweusi wa ‘plastiki’ (rambo), wengine walidai baada ya kutupa alikimbia na wananchi walipojaribu kumfukuza, polisi waliwarushia mabomu ya machozi, wengine walidai alikimbia na kuingia ndani gari jeupe aina ya Landrover TDI. Kila mmoja alikuwa na hadithi tofauti.
Hapo hospitali hakukuwa na kiongozi yeyote wa Serikali wala wa Jeshi la Polisi, isipokuwa baadhi ya viongozi wa CHADEMA pekee na wanachama wao waliokuwa wakiratibu shughuli zote, ikiwa ni pamoja na kutafuta damu kwa ajili ya majeruhi.
Hadi saa 4:30 usiku, majeruhi wote walikuwa wamepata huduma ya kwanza katika hospitali za Mount Meru, Selian na St. Elizabeth, na shughuli zote zilifanyika bila kiongozi hata moja wa Serikali kutokea.
Niliondoka eneo hilo nikiwa najiuliza maswali ambayo hadi sasa sijapata majibu yake. Nani anahusika na shambulio hilo? Kwa malengo gani? Nani kawatuma? Je; walengwa walikuwa viongozi wa CHADEMA? Tukio hilo linaashiria kuwa Arusha ambalo ni Jiji mashuhuri kwa utalii, likitoa ushindani mkali kwa majiji ya nchi nyingine kama Nairobi (Kenya), si salama tena kwa maisha ya watu na mali zao?
Kwa hakika, nimalizie kwa kumshukuru tena Mungu. Tukio hilo ni la kutisha, na waliohusika wana haki ya kulaaniwa. Kama si mapenzi ya Mungu, kuninusuru basi pengine, ningeweza kujeruhiwa vibaya au nami ningeuawa.
Nisingeweza kuonana tena na wanangu, mke wangu, ndugu na wanataaluma wenzangu na kwa kweli, kalamu yangu ingekuwa imefikia tamati. Lakini kwa mapenzi ya Mungu niko pamoja na natoa salamu za rambirambi kwa wote.
SIMULIZI HII IMEANDIKWA NA MWANDISHI PAUL SARAWATT KUTOK ARUSHA
No comments:
Post a Comment