Sunday, September 8, 2013

BINGWA VITUKO SHOW KING MAJUTO AFUNGUKA!!! TAZAMA MIAKA 55 YA UIGIZAJI NA AELEZA ALIVYOPATA JINA LA MAJUTO...



Dar es Salaam. Katika magazeti ya Mwananchi Wikiendi, tutakuletea mfululizo wa makala kuhusu mchekeshaji na mwigizaji nguli nchini Amri Athumani maarufu King Majuto, ambapo kwa kuanzia anaeleza alivyoanza kazi hiyo hata kuitwa Majuto. Endelea...

Umaarufu wa mtu hauji bila kuwepo sababu, kisa au chanzo hata kumfanya mhusika kutambulika na kujulika katika eneo fulani, jamii hata taifa.

Hili huwatokea watu katika fani au tasnia mbalimbali mfano siasa, uanaharakati, mchezo wa soka, filamu na maigizo.
Ndivyo ilivyo kwa Amri Athumani maarufu King Majuto, ambaye ni mwingizazi na mchekeshaji maarufu nchini anayetambulika na kutajwa kirahisi hata na watoto katika Tanzania hata nje ya mipaka yake.

Mchekeshaji na mwigizaji nguli nchini, Amri Athumani maarufu King Majuto  

Kwa maelezo yake, King Majuto amekuwa mwigizaji wa vichekesho kwa miaka 55 sasa, akijivunia mafanikio makubwa na kutambuliwa hata kimataifa.

Umaarufu wake ndiyo uliomsukuma mwandishi wa makala haya kufunga safari hadi eneo la Donge mkoani Tanga yalipo maskani ya Majuto ambaye hata ukimwona tu unaweza kucheka kutokana na vituko vyake vingi vyenye kuvutia na kufurahisha.

Alivyoanza kuigiza

Majuto anaeleza alivyoanza kuigiza akisema: “Nilianza kuigiza mwaka 1958 nikiwa na umri wa miaka 10. Nilikuwa darasa la pili, Shule ya Msingi ya Msembweni mkoani Tanga, kuna siku tukiwa darasani mlevi mmoja alikuwa akipita karibu na shule yetu, huku akipiga ngoma kwa nguvu.”

Anaongeza:”Mwanafunzi mmoja akajiunga kucheza huku mlevi yule akizidi kusogea na kuongeza mdundo, mwalimu aliyekuwa akifundisha alikasirika na kumtuma mwanafunzi mwingine kumfukuza yule mlevi, lakini badala ya kumfukuza mlevi na kumwita mwanafunzi anayecheza naye akajiunga kucheza.”

Anasema kuwa mwalimu alivyoona hivyo, alitoka nje ya darasa kwa kishindo na kwenda kumfukuza yule mlevi, lakini cha kushangaza wakati mwalimu alipomkaribia yule mlevi alianza kutingisha mabega yake kufuatisha mdundo ya ngoma, badala ya kumfukuza mlevi naye alijiunga na kuanza kucheza.

“Baada ya dakika tano kama shule nzima ilikuwa ikicheza ngoma, na baada ya hapo niliazimia kuwa msanii kwa kuwa sanaa ilimlainish hata mwalimu wetu aliyekuwa mkali kupita kiasi,” anasimulia Majuto.

Anaongeza kuwa mwaka 1966 alimaliza darasa la nane na mwaka uliofuatia alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ambapo walikuwa wakilipwa Sh20 na kufanya kazi hadi mwaka 1970, alipolazimika kuacha kwa sababu alikosa nafasi ya kufanya sanaa kama ndoto zake zilivyokuwa zikimtuma tangu utotoni.
Anaeleza kuwa hakuishia hapo kwani kabla ya kujikita rasmi kwenye sanaa pia aliwahi kufanya kazi Kikosi cha Zimamoto, Kiwanda cha Mabalanketi na Kampuni ya Bia Tanzania akiwa mlinzi.
Anabainisha kuwa mwaka 1976 ndipo alijiingiza rasmi kwenye sanaa na kuachana na kazi nyingine, ambapo kwa mara ya kwanza alikuwa akikusanya Sh6,000 kwa mwezi kutokana na kuigiza, kuimba na mambo mbalimbali ya utamaduni.
Anasimulia kwamba alianza uigizaji kwa kuigiza sauti za watu ambapo alikuwa akitengeneza mikanda ya kaseti iliyomlazimu kuifuta iwapo alikosea na haikuwa rahisi kusaihihisha tofauti na sasa.
“Aah, nimepata taabu mimi kuigiza. Nilikuwa natengeneza mikanda, nacheza sauti zote. Mmasai mimi, Wasukuma watani zangu mimi, Mchaga mimi, Mwarabu mimi kwani ndiyo makabila tuliyokuwa tukiigiza kipindi hicho. 
Nikikosea naanza tena, hadi nimalize, kazi ipo,”anaeleza akiongeza:
“Hapakuwa na soko kama sasa, ingawa hapakuwa na wizi wa kazi zetu, hakukuwa na hawa maharamia wa kuiba kazi za watu, kwa hiyo unakipata unachokifanyia kazi japo kidogo.”
Anafafanua kuwa kuna kipindi kaseti moja ilichukua wiki moja hata mwezi kukamilika, kwani studio hazikuwa na ubora wa sasa hivyo mwingiliano wa sauti ulikuwa mkubwa kiasi na kazi ilikuwa ngumu.
“Ndiyo maana nikiona mtu anachezea sanaa ananiudhi sana kwa kuwa nimeipatia taabu sana, pamoja na wenzangu wengi wanalikumbuka hili. Ukumbuke kuwa mimi ni mmoja wa wasanii wa mwanzo kutoa filamu ya vichekesho, hivyo adha ya kurekodi naijua sana,”anasema Majuto.

Alivyopata jina la Majuto
Majuto anaelezea kuwa baada ya kufanya kazi katika kampuni mblimbali, mwaka 1982 alijunga na Kundi la DDC Kibisa, ambapo kazi nyingi alizofanya zilikuwa za kusikitisha hata kuliza watu na ndpo lilipopatikana jina la King Majuto.
“Mashabiki ndiyo walinipa jina hili la King Majuto kwa maana ya Mfalme wa Kulia kwa kuigiza masikitiko, kipindi hicho sanaa ilikuwa ya majukwaani. Kuna kipindi nalia na kuliza wengine, si unajua tena, kumchekesha mtu ilivyo kazi, hata kumliza pia,”anasema Majuto.
Anasema kuwa baada ya kufanya kazi hiyo akiwa na vikundi mbalimbali mwaka 1985, alikwenda nchini Kenya ambako alikuwa akifanyia kazi zake katika Jiji la Nairobi na walianzisha kikundi kilichoitwa Golden Stars Accrobatic.
Kikundi hicho kiliundwa na vijana kutoka Tanga, yeye akiwa kiongozi wao, ambapo walikuwa wakifanya sanaa za maonyesho za majukwaani kwenye kumbi mbalimbali.
“Wale vijana walikuwa 11, walikuwa wakicheza vizuri na kwa ustadi mkubwa sarakasi na ngoma, hivyo nikawafanyia mpango wakaenda Marekani, nikabaki peke yangu. 
Nikaamua kurudi nyumbani na nilibaki kwa sababu sikuwa najua kucheza sarakasi, nikaona kuongozana nao nitaenda kuwa dobi wao bure wakati uwezo wa kuigiza nikiwa nyumbani ninao nikaamua kurudi,”anasema Majuto kwa mzaha.
Endelea kufuatilia mfululizo wa makala hii wiki ijayo kujua nini kilitokea kwa Majuto baada ya kurejea Tanzania .

No comments:

Post a Comment