Shughuli ya kutia saini mkataba wa amani kati ya waasi wa M23
na serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo,iliyokukuwa imepangwa kufanyika
Jumatatu , iligonga mwamba.
Hii ni kutokana na serikali ya Congo kusema kuwa mkataba huo uangaliwe upya
na hivyo kulazimisha shughuli hiyo kuahirishwa.Mpatanishi wa pande hizo mbili Ofuono Opondo wa Uganda, alisema kuwa pande hizo hazikuwa tayari kuonana ana kwa ana baada ya DRC kusema kuwa M23 watie saini mkataba katika chumba tofauti na kisha wapewe wao kuusaini.
Hata hivyo mpatanishi alisema haiwezekeni kwa hilo kufanyika kwa sababu pande zinazozozana lazima zikae katika chumba kimoja kwa ajili ya kufanikisha juhudi za upatanishi.
Kundi la waasi la M23 lilisitisha uasi wao baada ya kupata kipigo kutoka kwa wanajeshi wa DRC wakisaidiwa na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa waliowafurusha kutoka maficho yao ya milimani katika mpaka wa Rwanda na Uganda.
Mkataba huo ulistahili kutiwa saini mjini Kampala Uganda, ingawa shughuli yenyewe ilicheleweshwa bila ya kujua itafanyika lini.
Mwandishi wa BBC mjini Kampala, Ali Mutasa anasema kuwa mpatanishi mkuu Ofwono Opondo alisema mkataba hautatiwa saini na kwamba haijulikani ni lini makubaliano hayo yatasainiwa. Alisema Upande wa M23 uko tayari kwa shughuli hiyo na kuwa kizungumkuti kimetokana upande wa DRC.
Serikali ya DRC kupitia kwa msemaji wake,Lambert Mende ilisema kuwa Kinshasa iko tayari kutia saini makubaliano hayo, lakini sio mkataba unaosema ni makubaliano ya amani kwa sababu ni kama kundi hilo bado lipo.
Duru zinasema kuwa Rais Yoweri Museveni pamoja na wanadiplomasia wa nchi za Magharibi, walisubiri mkataba kutiwa saini lakini wajumbe wa DRC hawakuingia katika chumba cha hafla hiyo ya kutia saini.
No comments:
Post a Comment