Mhe. Tundu Lisu |
KUHUSU
MUSWADA WA SHERIA YA MAREKEBISHO YA SHERIA
YA MABADILIKO YA KATIBA (NA. 2), YA MWAKA 2013
(Kanuni ya 86(6) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2013)
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Tumerudi kwa mara nyingine tena kutafakari mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ya Sheria za Tanzania. Hii ni mara ya tatu kwa Bunge lako tukufu kufanya hivyo kuhusiana na Sheria hii hii. Kama itakavyokumbukwa, marekebisho ya kwanza yalifanyika mwezi Februari ya mwaka jana, wakati marekebisho ya pili yalifanyika aghalabu mwezi mmoja na nusu uliopita.
Mara hii, kama ililvyokuwa kwa Sheria mama wakati wa Mkutano wa Tatu wa Bunge hili tukufu mwezi Aprili, 2011, Muswada wa Sheria ya Marekebisho umeletwa kwenye Bunge lako tukufu kwa Hati ya Dharura ya Mheshimiwa Rais ya tarehe 28 Oktoba, 2013. Muswada huu ulichapishwa kwenye Gazeti la Serikali la siku tatu kabla, yaani tarehe 25 Oktoba, 2013. Hii ina maana kwamba, kwa mujibu wa kanuni ya 93(3) ya Kanuni za Kudumu na kwa mujibu wa ratiba mpya ya Mkutano huu wa Bunge lako tukufu, Muswada huu unatakiwa ujadiliwe na kupitishwa leo hii hii.
Mheshimiwa Spika,
Kama tulivyosema wakati wa kujadili Muswada wa Sheria ya Uendeshaji Mahakama wakati wa Mkutano wa Tatu wa Bunge lako tukufu, matumizi ya Hati ya Dharura katika utungaji wa sheria yana madhara makubwa na ya wazi kwa demokrasia yetu: “... [S]heria zinazotungwa haraka haraka namna hiyo zinakosa uhalali wa kisiasa kwa sababu ya kukosa ushiriki wa Wabunge na wadau wengine. Vile vile, sheria hizo zinakuwa na makosa mengi kwa sababu ya kukosekana umakini katika kuzitunga na utekelezaji wake kisiasa na kisheria unakuwa mgumu. Aidha, sheria za aina hiyo zinafisha demokrasia na uwajibikaji wa Serikali kwa Bunge na kwa wananchi kwa sababu jukumu la kikatiba la Bunge kama baraza la kutunga sheria na la kusimamia serikali linageuzwa kuwa ni la kupiga muhuri maamuzi na mapendekezo yanayoletwa na Serikali. Mwishowe, Bunge la aina hiyo linakosa hadhi na heshima kwa wananchi na hivyo kukaribisha aina nyingine za siasa za nje ya Bunge.” Historia ya miaka miwili ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inathibitisha ukweli wa kauli hii.
Mheshimiwa Spika,
Kama ilivyokuwa kwa marekebisho ya kwanza ya Sheria hii, Muswada huu umekuja kufuatia Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati kufuatia mtafaruku uliotokea wakati wa, na baada ya, kupitishwa kwa marekebisho ya pili ya Sheria hii wakati wa Mkutano uliopita wa Bunge lako tukufu. Mara hii Mheshimiwa Rais aliwaita viongozi wakuu wa vyama vya siasa vyenye uwakilishi Bungeni kwenye majadiliano yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, tarehe 15 Oktoba, 2013. Baadaye, kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, viongozi wakuu wa vyama hivyo walikutana chini ya uratibu wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) mnamo tarehe 17 na 20 Oktoba, 2013, ili kukubaliana juu ya maeneo ya Sheria hii yanayohitaji kurekebishwa kwa ajili ya kuyawasilisha serikalini. Muswada huu ni matokeo ya mchakato huo.
Mheshimiwa Spika,
Muswada huu unapendekeza marekebisho katika vifungu vitatu vya Sheria na Sehemu ya VI ambayo vifungu vyake vikuu vitafutwa na kutungwa upya katika Sheria ya Kura ya Maoni, ambayo Muswada wake unaanza kujadiliwa leo hii hii. Maeneo yanayopendekezwa kurekebishwa yanahusu idadi ya wajumbe wa Bunge Maalum wasiotokana na Wabunge, mamlaka na utaratibu wa uteuzi wao; mamlaka ya Makatibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi kufanya maandalizi kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Bunge Maalum na utaratibu wa kufanya maamuzi juu ya Rasimu ya Katiba katika Bunge hilo. Eneo la mwisho linalopendekezwa kurekebishwa ni utaratibu wa uhalalishaji wa Katiba Mpya katika Sehemu ya VI ya Sheria.
1. IDADI YA WAJUMBE WA BUNGE MAALUM
Mheshimiwa Spika,
Muswada unapendekeza kuongeza idadi ya wajumbe wa Bunge Maalum wasiotokana na Wabunge na Wawakilishi kutoka mia moja sitini na sita walioko kwa mujibu wa kifungu cha 22(1)(c) cha Sheria ya sasa hadi kufikia wajumbe mia mbili na moja. Hili ni ongezeko la wajumbe thelathini na tano na litafanya idadi ya wajumbe wote wa Bunge Maalum kufikia mia sita thelathini na tisa. Kama ilivyokuwa tangu Sheria hii ilipotungwa mwaka 2011, wajumbe hawa watateuliwa na Rais kwa makubaliano na Rais wa Zanzibar.
Licha ya mabadiliko ya idadi yao, kuna mapendekezo mengine ya marekebisho yanayohusu wajumbe wa Bunge Maalum. Wakati Sheria ilitamka tu kwamba wajumbe hao watatokana na makundi tisa yaliyoainishwa katika kifungu cha 22(1)(c) bila kufafanua taasisi husika za kila kundi wala idadi ya wajumbe kwa kila kundi, aya ya 2(a) ya Muswada inapendekeza idadi ya wajumbe kwa kila kundi lililotajwa katika kifungu hicho. Hivyo, kwa mfano, kundi la taasisi zisizokuwa za kiraia litawakilishwa na wajumbe ishirini; taasisi za kidini zitawakilishwa na wajumbe ishirini, na vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu vitawakilishwa na wajumbe arobaini na mbili.
Makundi mengine ni taasisi za elimu ya juu ambazo zitawakilishwa na wajumbe ishirini; makundi ya watu wenye mahitaji maalum wajumbe ishirini, na vyama vya wafanyakazi ambavyo vitawakilishwa na wajumbe kumi na tisa. Mengine ni vyama vinavyowakilisha wafugaji vitakavyowakilishwa na wajumbe kumi; wajumbe kumi kutoka vyama vya wavuvi; wajumbe ishirini kutoka vyama vya wakulima, na wajumbe ishirini kutoka makundi mengine yoyote ya watu wenye maslahi yanayofanana.
Aya ya 2(b) ya Muswada inamtaka Rais kuyaalika makundi hayo kutoka pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano kumpelekea orodha ya majina ya watu wasiopungua sita na wasiozidi tisa kwa ajili ya kufikiriwa kuteuliwa kuwa wajumbe wa Bunge Maalum. Kwa kila jina litakalopendekezwa, kutaonyeshwa umri, jinsia, uzoefu, ujuzi na mahali anapoishi mhusika. Na katika kufanya uteuzi kutokana na majina hayo, Rais atatakiwa kutilia maanani uwiano wa kijinsia.
Mheshimiwa Spika,
Mapendekezo ya marekebisho haya ni mapya na kwa kiasi fulani ni hatua chanya ikilinganishwa na Sheria kama ilivyo sasa. Kwanza, ongezeko lolote la wajumbe wasiokuwa Wabunge na Wawakilishi linapunguza hodhi ya vyama vya siasa kwa mchakato wa Katiba Mpya. Hii ni kwa sababu, sifa mojawapo kuu ya Wabunge au Wawakilishi wa aina zote ni kwamba wote wametokana na ni wanachama wa vyama vya siasa.
Pili, kwa kuweka idadi ya wajumbe watakaowakilisha kila kundi lililotajwa na kifungu cha 22(1)(c) cha Sheria, kuna uwezekano mkubwa zaidi wa makundi hayo kuwakilishwa katika Bunge Maalum kuliko ambavyo idadi ya kila kundi isingewekwa wazi. Tatu, kwa sababu ya ongezeko la wajumbe wasiokuwa Wabunge na Wawakilishi, kuna uwezekano mkubwa zaidi wa mjadala katika Bunge Maalum kuwa bora zaidi kwa kuingiza sauti na mitazamo isiyotawaliwa na maslahi ya kivyama. Yote haya yanaongeza uwezekano wa kupatikana Katiba Mpya yenye taswira ya Kitanzania zaidi badala ya Katiba yenye taswira ya kivyama zaidi na hayana budi kuungwa mkono.
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, mapendekezo haya bado hayajatosheleza haja ya kuwa na mchakato wa kidemokrasia zaidi na wenye kujenga maridhiano ya kitaifa katika kutengeneza Katiba Mpya. Kwanza, kwa kuendelea kumng’ang’aniza Rais kuwateua wajumbe hawa, Muswada huu unaendeleza dhana ya Urais wa Kifalme katika mchakato wa Katiba Mpya. Tumeielezea dhana hii kwa kirefu kuhusiana na mchakato huu kiasi kwamba hatuna haja ya kujirudia rudia hapa. Itoshe tu kukumbushia kwamba hata Chama cha Mapinduzi (CCM) katika enzi za ujana wake kilikuwa kinatambua hatari ya Urais wa Kifalme katika mfumo wa kikatiba na kisheria wa nchi yetu. Ndio maana katika Mwongozo wake wa 1981, CCM ililalamika kwamba “madaraka mengi na makubwa yamelimbikizwa katika Ofisi ya Rais.”
Ukweli ni kwamba hata Rais Kikwete mwenyewe ameonyesha dhahiri kwamba hataki mamlaka haya ambayo Muswada huu unamng’ang’aniza. Katika mkutano wake na viongozi wakuu wa vyama vya siasa, Mheshimiwa Rais alisema kwamba alikuwa tayari kuyaachia makundi yaliyotajwa katika kifungu cha 22(1)(c) kuteua wawakilishi wao wenyewe endapo vyama vya siasa vingekubaliana juu ya formula ambayo ingehakikisha uwiano mzuri wa jinsia unazingatiwa. Ndiyo maana vyama vya siasa vyenye uwakilishi ndani ya Bunge hili vilikubaliana kwamba “kifungu cha 22(2A) cha Sheria kama ilivyo sasa kifutwe kabisa ... (na) kwamba wajumbe waliotajwa katika kifungu cha 22(1)(c) watateuliwa na taasisi watakazoziwakilisha.”
Pili, kwa kutaja makundi ya jumla badala ya kutaja taasisi zinazounda makundi hayo, Muswada unatoa mwanya kwa Rais kuteua watu anaowataka yeye na kueleza kwamba wametokana na kundi mojawapo ya yale yaliyotajwa katika kifungu cha 22(1)(c) cha Sheria. Kwa kiasi fulani, hivyo ndivyo ilivyotokea wakati wa mchakato wa kuteua wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kwa kadri ya taarifa zilizotolewa na wadau mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge lako tukufu ya Katiba, Sheria na Utawala wakati wa kujadili marekebisho ya pili ya Sheria hii mwezi Agosti mwaka huu.
Tatu, hata kama majina atakayopelekewa Rais hayatachakachuliwa, mapendekezo ya aya ya 2(b) hayawezi kutekeleza matakwa ya kuwa na wajumbe mia mbili na moja wanaopendekezwa kwenye aya ya 2(a) ya Muswada huu. Hii ni kwa sababu aya hiyo inapendekeza Rais apelekewe majina yasiyopungua sita na yasiyozidi tisa kutoka kila kundi lililotajwa katika kifungu cha 22(1)(c) kutoka sehemu mbili za Jamhuri ya Muungano.
Assuming, kama aya ya 2(b) inavyoashiria, kwamba kila sehemu ya Jamhuri ya Muungano ina makundi yaliyotajwa katika kifungu hicho, kutakuwa na makundi ishirini yatakayotakiwa kupeleka majina kati ya sita na tisa kwa Rais kwa ajili ya uteuzi. Sasa endapo kila moja ya makundi hayo litapeleka idadi ya juu kabisa inayopendekezwa na Muswada; na endapo wajumbe wote hao watateuliwa kuwa wajumbe wa Bunge Maalum, idadi yao itakuwa mia moja themanini. Kutakuwa na baki ya wajumbe ishirini na moja ambao haijulikani watatoka wapi.
Kwa upande mwingine, endapo kila kundi lililotajwa litapeleka idadi ya chini kabisa ya majina kama inavyopendekezwa; na idadi hiyo wakateuliwa wote bila kuacha hata mmoja, basi idadi ya wajumbe wa Bunge Maalum wasiotokana na Bunge au Baraza la Wawakilishi itakuwa mia moja na ishirini. Kutakuwa bado na akiba ya wajumbe themanini na moja ambao haijulikani watapatikana wapi na kwa utaratibu gani. Kwa vyovyote vile linavyoangaliwa, pendekezo la aya ya 2(b) haliwezi kutekeleza matakwa ya pendekezo la aya ya 2(a) ya Muswada huu kuhusu idadi ya wajumbe wa Bunge Maalum wasiokuwa Wabunge na Wawakilishi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza namna tatu za kutatua tatizo hili. Njia ya kwanza ni kufuta kabisa pendekezo la Rais kupelekewa kati ya majina sita hadi tisa kwa ajili ya uteuzi. Badala yake, aya ya 2(b) ipendekeze kwamba Rais apelekewe na makundi husika majina kulingana na idadi iliyopangwa kwa kila moja ya makundi yaliyotajwa na kifungu cha 22(1)(c) cha Sheria. Hii itahakikisha kwamba idadi ya wajumbe mia mbili na moja inayopendekezwa inafikiwa.
Kwa wanaopendekeza kivuli kikubwa cha Rais katika mchakato wa Katiba Mpya kiendelee, pendekezo hili litamwondolea Rais discretionaliyo nayo katika kuteua wajumbe hao wa Bunge Maalum. Badala yake, kazi ya Rais itakuwa ni mere formality kwa maana kwamba atateua wajumbe kutokana na idadi kamili atakayopatiwa na kila kundi.
Namna ya pili ya kutatua tatizo lililoletwa na pendekezo la aya ya 2(b) ya Muswada ni kufanya idadi ya majina atakayopelekewa Rais kuwa kubwa zaidi ya idadi ya wajumbe wa kila kundi. Hivyo, kwa mfano, kundi la taasisi zisizo za kiserikali, au za kidini, au taasisi za elimu ya juu, litapeleka majina kati ya thelathini hadi arobaini ili Rais ateue wajumbe ishirini wa kundi hilo kama inavyopendekezwa na aya ya 2(a). Aidha, kwa makundi ya vyama vya wafanyakazi, au wakulima, au wafugaji nayo yatapeleka majina mengi zaidi ya mgawo wao ili Rais aweze kuteua idadi ya wajumbe inayotakiwa kwa kila kundi.
Pendekezo hili litahifadhi mamlaka substantive ya uteuzi aliyo nayo Rais, lakini litathibitisha dhana kwamba wajumbe hao ni watu wa Rais badala ya kuwa wawakilishi wa makundi yaliyowapendekeza.
Njia ya tatu ya kutatua tatizo la namna ya kuwapata wajumbe wa Bunge Maalum waliotajwa katika aya ya 2(a) ya Muswada ni kuzitaja taasisi zinazounda makundi hayo na kuzigawia idadi ya wajumbe watakaoteuliwa kutoka kila taasisi. Hapa inawezekana kila taasisi iliyotajwa kupeleka majina kulingana na idadi ya wajumbe iliyotengewa, kama ulivyo msimamo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni; au kupeleka idadi kubwa zaidi ya majina kuliko idadi ya wajumbe wa kutoka taasisi hiyo, na hivyo kumpa Rais flexibility ya kuteua anavyoona yeye inafaa, kama inavyopendelewa na Serikali. Sehemu ya kwanza ya pendekezo hili ilikwishakubaliwa na wakuu wa vyama vinavyounda TCD lakini ikakataliwa na Serikali. Huu ni wakati muafaka wa kulifikiria tena pendekezo hili.
2. HOJA YA GHARAMA ZA BUNGE MAALUMMheshimiwa Spika,
Serikali hii ya CCM imetumia hoja mbili kukataa kuongeza idadi ya wajumbe wa Bunge Maalum. Kwanza, inadaiwa kwamba ongezeko la wajumbe, kama ilivyopendekezwa na wadau wengi, litaongeza gharama za Bunge Maalum katika nyakati hizi za ‘Sungura Mdogo’ na economic belt-tightening. Pili, inadaiwa kwamba Ukumbi huu wa Bunge lako tukufu – unaotazamiwa kuwa venue ya Bunge Maalum – hautatosha endapo idadi ya wajumbe itaongezeka kama inavyopendekezwa.
Mheshimiwa Spika,
Mchakato wowote wa maana wa kutengeneza Katiba Mpya huwa na gharama kubwa. Hii ni kweli kwa nchi zote ambazo zimepitia mchakato huo, na itakuwa kweli kwa Tanzania pia. Kama Waheshimiwa Wabunge watakavyokumbuka, tangu mchakato huu uanze kwa uteuzi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mei Mosi 2012, Bunge lako tukufu limekwishaidhinisha zaidi ya shilingi bilioni 74.463 kwa ajili ya shughuli za Tume peke yake. Kwa vyovyote vile itakavyokuwa, shughuli za Bunge Maalum zitakuwa na gharama kubwa pia, kama sio zaidi.
Pamoja na ukweli huu, hoja zote mbili za Serikali hii ya CCM ni potofu. Kwanza, hadi sasa, licha ya kutakiwa kufanya hivyo katika Mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge la Bajeti, Serikali haijatangaza – na wala Bunge lako tukufu halijaidhinisha – bajeti yoyote ya Bunge Maalum. Kwa sababu hiyo, hakuna msingi wala ushahidi wowote wa kupima ukweli na uhalali wa hoja ya ongezeko kubwa la gharama linalodaiwa na Serikali hii ya CCM endapo wajumbe wa Bunge Maalum wataongezwa kama ilivyopendekezwa na wadau mbali mbali, wakiwamo vyama vyetu vya siasa. Vinginevyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM ilieleze Bunge lako tukufu na Watanzania kwa ujumla makadirio ya gharama za shughuli za Bunge Maalum. Aidha, Serikali ieleze gharama hizo zimeidhinishwa na kikao kipi cha Bunge lako tukufu.
Pili, licha ya ukweli wa gharama kubwa za kutengeneza Katiba Mpya, gharama za mchakato mbovu ni kubwa zaidi. Gharama hizo hazijumuishi fedha, muda na rasilmali nyingine peke yake, bali pia zinaweza kujumuisha uharibifu mkubwa wa mali na uchumi, na hata upotevu wa maisha ya watu, endapo maridhiano na muafaka wa kitaifa havitapatikana na nchi ikaingia katika mtafaruku na machafuko ya kisiasa.
Kwenye jambo hili hatuna budi kujifunza kutoka kwa majirani zetu wa Kenya ambapo Rais wa nchi hiyo na Makamu wake wanakabiliwa na mashtaka ya makosa dhidi ya ubinadamu katika Mahakama ya Jinai ya Kimataifa, The Hague, kufuatia vurugu za kisiasa zilizosababishwa na machafuko ya Uchaguzi Mkuu wa Desemba, 2007. Uchaguzi huo ulifanyika baada ya mchakato wa Katiba Mpya ya nchi hiyo kuvunjika mwaka 2006 pale Rasimu ya Katiba Mpya ilipokataliwa na Wakenya kwenye kura ya maoni. Matokeo yake, maelfu ya watu waliuawa au kujeruhiwa, mabilioni ya fedha na mali kuteketea na jumuiya ya kimataifa kuingilia kati kabla Wakenya hawajafunguka macho kwamba kujenga muafaka wa kitaifa juu ya Katiba Mpya ni gharama nafuu zaidi kuliko kiasi chochote cha fedha!
Tatu, hoja ya udogo wa Ukumbi kwa ajili ya Bunge Maalum ni ya kuchekesha. Kwanza, tangu kuzaliwa kwake zaidi ya miaka thelathini na sita iliyopita, CCM imefanyia Mikutano yake yote Mikuu hapa Dodoma. Hata vyama vya upinzani kama CHADEMA na CUF navyo vimefanya Mikutano yao Mikuu au Mabaraza ya Taifa hapa hapa nchini. Mikutano na Mabaraza hayo ina mamia na hata maelfu ya wajumbe na suala la udogo wa kumbi za kuifanyia halijawahi kuizuia isifanyike.
Pili, hoja hii inapingana moja kwa moja na kauli ya Katibu wa Bunge lako tukufu kwa vyombo vya habari kwamba Ukumbi huu utawekewa viti vingine 750 “ambavyo vitatosha ukumbini hapo bila kubanana.” Na hata kama bado hautatosha kwa ajili ya idadi ya wajumbe wa Bunge Maalum wanaopendekezwa na wadau, basi ukumbi mwingine mkubwa zaidi unaweza kutafutwa hapa hapa Dodoma na hata nje ya Dodoma kama ikihitajika. Muafaka wa kitaifa juu ya Katiba Mpya ni muhimu zaidi kuliko gharama za ukumbi wa mikutano.
3. MAKATIBU WA BUNGE MAALUMMheshimiwa Spika,
Aya ya 3(a) ya Muswada inapendekeza kumpa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar mamlaka ya kufanya “... maandalizi muhimu kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Bunge Maalu.” Katika haraka haraka ya kupitisha marekebisho ya pili ya Sheria hii, suala hili halikuwekwa kwenye Muswada na hivyo halikufikiriwa na Bunge lako tukufu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaunga mkono pendekezo hili.
4. HATIMA YA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Sheria kama ilivyo sasa, Tume ya Mabadiliko ya Katiba itavunjwa na Rais “baada ya kuwasilishwa kwa Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalum....” Hata hivyo, kwa mujibu wa kifungu kipya cha 20(4) cha Sheria, “... Katibu wa Bunge Maalum anaweza, kwa kushauriana na Mwenyekiti wa Bunge Maalum, kumwalika Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti au Mjumbe yeyote wa Tume iliyovunjwa ili kutoa ufafanuzi utakaohitajika wakati wa mjadala wa Bunge Maalum.”
Licha ya matakwa haya ya Sheria kama ilivyo sasa, kifungu cha 33(2) cha Sheria hiyo hiyo kinailazimisha Tume “... kutoa elimu ya uraia na uhamasishaji juu ya Katiba inayopendekezwa kwa muda usiozidi siku thelathini kuanzia siku ya kuchapishwa (kwa taarifa ya kura ya maoni) katika Gazeti la Serikali.” Hii ni kwa “madhumuni ya kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuhusu kuipigia kura ya maoni Katiba inayopendekezwa....” Aidha, sambamba na kifungu cha 33(2) cha Sheria, Bunge lako tukufu limetenga mabilioni ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu haya ya Tume katika mwaka huu wa fedha wa 2013/2014.
Mheshimiwa Spika,
Pendekezo la kuivunja Tume mara tu baada ya kuwasilisha ripoti yake na Rasimu ya Katiba kwa Rais halikuwa sehemu ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho iliyopitishwa katika Mkutano uliopita wa Bunge lako tukufu. Kwa mujibu wa Taarifa Rasmi ya Majadiliano ya Bunge (Hansard) ya tarehe 6 Septemba, 2013, hoja hiyo ililetwa Bungeni na Mheshimiwa Selemani Jafo. Katika hoja yake, Mheshimiwa Jafo alidai kwamba pendekezo hilo “... ni kutokana na kilio cha Watanzania wengi waliokuwa wanapiga kelele mpaka wengine kuwavunjia heshima wazee wetu ambao kwa kweli wapo tu....”
Taarifa hiyo ya Hansard inaonyesha kwamba hoja ya Mheshimiwa Jafo iliungwa mkono na Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Mathias Chikawe kwa maneno yafuatayo: “Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili Mheshimiwa Jafo wala asipoteze nguvu nyingi sana kulisemea, kwa sababu na mimi naliona na ninakubali kwa sababu ... inawezekana ilikuwa tu ni oversight kwa upande wetu tulipokuwa tunatunga hii sheria. Haiwezekani Tume ikaendelea bila kuvunjwa.” Taarifa hiyo inaonyesha vile vile kwamba hoja ya Mheshimiwa Jafo iliungwa mkono pia na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Mheshimiwa Spika,
Katika hotuba yake kwa wananchi ya tarehe 4 Oktoba, 2013, Rais Kikwete aliisifu kazi ambayo Tume imeifanya kwa maneno yafuatayo: “Bahati nzuri (kutengeneza Katiba ya watu wa vyama vyote na wasiokuwa na vyama ambao ndio wengi kuliko wote) ndio sifa kubwa iliyoonyeshwa na wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Wamewasimamia na kuwasemea watu wote bila ya kubagua. Natambua kuwepo kwa baadhi ya watu ambao hawafurahii msimamo huo na matokeo ya kazi yao. Watu hao kuwalaumu wajumbe wa Tume kwa ajili hiyo ni kutowatendea haki.”
Akizungumzia uhai wa Tume, Mheshimiwa Rais alisema yafuatayo: “Katika orodha ya madai ya ndugu zetu wa upinzani lipo suala la uhai wa Tume ya Katiba. Wanataka usiishe wanapokabidhi rasimu ya pili kwa Bunge Maalum bali waendelee kuwepo mpaka mwisho wa mchakato. Nimeulizia ilikuwaje? Nimeelezwa kuwa jambo hili halitokani na mapendekezo ya Serikali wala ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala. Limetokana na pendekezo la Mbunge katika Bunge wakati wa kupitia vifungu na kuungwa mkono na Wabunge wengi. Kwa hiyo kuilaumu Serikali si haki. Serikali inaweza kuwa mshirika katika hoja hii. Name naiona hoja ya Wajumbe wa Tume kuwa na wajibu wakati wa Bunge Maalum hasa wa kusaidia kufafanua mapendekezo ya Tume.”
Kama Mheshimiwa Rais mwenyewe anaiona ‘hoja ya wajumbe wa Tume kuwa na wajibu wakati wa Bunge Maalum hasa wa kusaidia kufafanua mapendekezo ya Tume’, haitaeleweka endapo Bunge lako tukufu litakataa kufanya marekebisho ya Sheria hii ili kuiwezesha Tume kuendelea kuwepo kama ilivyokuwa kabla marekebisho ya pili hayajapitishwa. Kwa sababu hizo, na kama walivyokubaliana viongozi wakuu wa vyama vya kibunge, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kama ifuatavyo kuhusu hatima ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba:
a) Kifungu cha 20(4) cha Sheria kifutwe kabisa;(b) Kifungu cha 22(1) kirekebishwe kwa kuongeza aya ya (d) mara baada ya aya (c) itakayosomeka kama ifuatavyo: “Wajumbe wa Tume ambao hawatakuwa na haki ya kupiga kura katika Bunge Maalum, yaani watakuwa wajumbe ex officio wa Bunge Maalum.”
(c) Kifungu cha zamani cha 37(1) kirejeshwe ili kuwezesha uwepo wa Tume hadi baada ya matokeo ya kura ya maoni kutangazwa kama ilivyokuwa kabla ya marekebisho ya pili ya Sheria hii.
5. UTARATIBU WA KUPITISHA VIFUNGU VYA KATIBA MPYA
Mheshimiwa Spika,
Aya ya 4 ya Muswada huu inapendekeza kufutwa kwa vifungu vidogo vya (3), (4), (5), (6) na (7) vya kifungu cha 26 ambavyo viliingizwa na marekebisho ya pili. Vifungu hivyo vilikuwa na athari ya kuruhusu Katiba Mpya kupitishwa kwa wingi wa kawaida wa wajumbe wa Bunge Maalum. Mapendekezo ya marekebisho ya kifungu yana athari ya kurudisha status quo ante, yaani hali kama ilivyokuwa kabla ya marekebisho ya pili ya Sheria hii. Kwa maana hiyo, endapo mapendekezo haya yatakubaliwa na Bunge lako tukufu, Katiba Mpya itaamuliwa kwa wingi maalum wa theluthi mbili ya wajumbe wote wa Bunge Maalum wanaotoka Tanganyika na idadi hiyo hiyo ya wajumbe wanaotoka Zanzibar. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayakubali mapendekezo haya na inawasihi Waheshimiwa Wabunge wote wayaunge mkono.
6. UHALALISHAJI WA KATIBA MPYAMheshimiwa Spika,
Aya ya 5 ya Muswada inapendekeza kufutwa kwa vifungu sita vya Sehemu ya Sita ya Sheria inayohusu uhalalishaji wa Katiba Mpya. Kama tulivyosema awali, vifungu vinavyofutwa vimehamishiwa katika Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni, 2013. Vifungu viwili vinavyopendekezwa kubaki ni kifungu cha 37 kinachohusu kuvunjwa kwa Tume na ambacho tumekwishakijadili kwa kirefu; na kifungu cha 38 kinachohusu kuanza kutumika kwa Katiba Mpya. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakubaliana na mapendekezo ya marekebisho haya na inasihi Waheshimiwa Wabunge wote wayaunge mkono.
Mheshimiwa Spika, Baada ya kusema yote haya naomba kuwasilisha.
Tundu Antiphas Mughwai Lissu (MB)
MSEMAJI, KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
&
WAZIRI KIVULI, KATIBA NA SHERI
No comments:
Post a Comment