Tuesday, November 12, 2013

Wanawake wananyanyaswa zaidi Misri


Wanawake wa Misri wakishiriki maandamano
 
Misri inasemekana kuwa nchi yenye rekodi mbaya zaidi ya haki za wanawake katika mataifa ya kiarabu. Hii ni kwa mujibu wa kura ya maoni iliyofanywa na wataalamu wa maswala ya kijinsia.
 
Utafiti huo uligundua kuwa wanawake wanadhulumiwa sana kingono, visa vingi vya ukeketaji wa wasichana na ongezeko la makundi ya watu wenye itikadi kali kuwa baadhi ya mambo yanayochangia dhuluma dhidi ya wanawake.

 
Visiwa vya Comoros vilishikilia nafasi ya kwanza katika utafiti huo uliofanywa na wakfu wa Thomson Reuters.
Zaidi ya wataalamu 330 wa maswala ya jinsia walihojiwa katika nchi 21 za kiarabu ikiwemo Syria.
Huu ni utafiti wa tatu wa aina hii kufanywa na wakfu huo uliolenga hasa haki za wanawake tangu harakati za mapinduzi kuanza kushuhudiwa katika nchi za kiarabu mwaka 2011.

'unyanyasaji kila siku'

Iraq ilishikilia nafasi ya pili baada ya Misri ikifuatiwa na Saudi Arabia, Syria na Yemen kuwa miongoni mwa nchi zenye rekodi mbovu kuhusu haki za wanawake.
Nchini Comoros ambako wanawake wanashikilia asilimia 20 ya nyadhifa za mawaziri, inafuatiwa na Oman, Kuwait, Jordan na Qatar.
Kura ya maoni iliwataka wataalamu kutathmini maswala kama dhulumua dhidi ya wanawake, haki za afya ya uzazi , ambavyo wanawake wanatendewa katika familia na jukumu la wanawake katika siasa na uchumi.
Sheria zinazochochea ubaguzi dhidi ya wanawake pamoja na biashara haramu ya binadamu ndizo sababu zilizochangia Misri kuwa na rekodi mbaya zaidi katika ambavyo wanawake wanatendewa katika nchi 22 za kiarabu.

Nchini Misri kuna sehemu ambazo shughuli za kiuchumi na biashara zinazingatia sana biashara haramu ya kuwauza wanawake na kuwafanyisha ndoa za lazima.

Hata hivyo dhuluma za kingono ndio changamoto kubwa zaidi dhidi ya wanawake.
Ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa mnamo mwezi Aprili ilisema kuwa asilimia 99.3 ya wanawake wamedhulumiwa kingono.

Wakati huo huo, Iraq imesemekana kuwa mahala hatari sana kwa wanawake kuishi kuliko ilivyokuwa chini ya utawala wa hayati Saddam Hussein..

No comments:

Post a Comment