Siku nne baada ya Kimbunga Haiyan kupiga mji wa Tacloban
,Ufilipino, maelfu ya watu wangali wanasubiri msaada wa dharura.
Umoja wa mataifa umetoa wito kwa jamii ya kimataifa kutoa msaada wa dola
millioni 301 ili kuwasaidia watu nchini Ufilipino.Wakati huohuo, Meli za Marekani na Uingereza zinaelekea nchini Ufilipino huku Umoja wa Mataifa ukiomba msaada kupelekwa nchini humo kukiwa na taarifa za uharibifu mkubwa uliosababishwa na kimbunga Haiyan.
Marekani imepeleka ndege na meli za mizigo kwenda Ufilipino, wakati ambapo Uingereza imepeleka meli ya kivita.
Watu wapatao 10,000 wanahofiwa kufa, na maelfu ya walionusurika katika kimbunga Haiyan wanahitaji msaada.
Rais wa Ufilipino Benigno Aquino ametangaza hali hiyo kuwa janga la kitaifa.
Katika taarifa yake, Rais Aquino,amesema majimbo mawili ya Leyte na Samar yameathirika zaidi kutokana na kimbunga hicho, ikiwemo watu wengi kupoteza maisha.
Juhudi kubwa za kimataifa zinafanyika ili kutoa msaada wa dharura kwa Ufilipino, lakini wafanyakazi wa mashirika ya kutoa msaada wanakwama kuyafikia maeneo yaliyokumbwa na kimbunga.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amezielezea picha zinazoonyesha ya kimbunga hicho kuwa zinatisha na kukatisha tamaa.
Umoja wa Mataifa utazindua mpango mkubwa wa msaada wa kibinadamu, na kutenga dola milioni 25 kusaidia jitihada za misaada ya dharura.
"Maelfu ya watu wameripotiwa kufa na watu wapatao milioni kumi wameathirika kutokana na kimbunga hicho. Hebu tuonyeshe mshikamano wetu na watu wa Ufilipino katika kipindi hiki cha kuhitaji msaada," amesema.
Mbali na Marekani na Uingereza, nchi nyingine pia zimeahidi mamilioni ya dola ukiwa ni msaada kwa Ufilipino. Australia imeidhinisha dola milioni 9, wakati ambapo New Zealand imeahidi zaidi ya dola milioni moja, huku Uchina ikiahidi kutoa dola laki moja.($100,000)
No comments:
Post a Comment