Thursday, May 1, 2014

MRADI WA HAKUNA WASICHOWEZA WATOA ELIMU NA MISAADA YA VIFAA VYA KUJISITIRI WAKATI WA HEDHI KWA WASICHANA 6000 MKOANI MTWARA

Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara Bw. Salum Masalanga (katikati) akikabidhi msaada wa pedi kwa Mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya Maendeleo, Neema Mohamed chini ya programu ya Hakuna Wasichoweza iliyofadhiliwa na Vodacom na T-MARC. Wakishuhudia tukio hilo, ni Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Jamii Vodacom, Yesaya Mwakifulefule (kushoto)na Mratibu wa Mradi kutoka T-MARC Tanzania, Bi. Dorice Chalambo (kulia), mradi huo umeanza kufanya kazi mkoa wa Mtwara na Lindi na kusambaa nchi nzima.
Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara Bw. Salumu Masalanga (katikati) akipokea msaada wa pedi kwa niaba ya wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Maendeleo chini ya programu ya Hakuna Wasichoweza iliyofadhiliwa na Vodacom na T-MARC. Wakishuhudia tukio hilo, ni Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Jamii Vodacom, Yesaya Mwakifulefule (kushoto) na Mratibu wa Mradi kutoka T-MARC Tanzania, Bi. Dorice Chalambo (wa pili kulia), mradi huo umeanza kufanya kazi mkoa wa Mtwara na Lindi na kusambaa nchi nzima.
Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Jamii Vodacom, Yesaya Mwakifulefule (kushoto) na Mratibu wa Mradi kutoka T-MARC Tanzania, Bi. Dorice Chalambo (wa pili kulia) kwa pamoja wakikabidhi msaada wa pedi kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Maendeleo chini ya programu ya Hakuna Wasichoweza iliyofadhiliwa na Vodacom na T-MARC. Akishuhudia tukio hilo (katikati) ni Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara Bw. Salumu Masalanga, mradi huo umeanza kufanya kazi mkoa wa Mtwara na Lindi na kusambaa nchi nzima.

Wasichana wa mkoani Mtwara wamefaidika na elimu ya afya pamoja na vifaa vitakavyowasaidia kujisitiri wakati wa hedhi. Elimu hii na msaada vimetolewa kupitia mradi wa Hakuna Wasichoweza unaotekelezwa na asasi ya T-MARC Tanzania. 

Mradi wa Hakuna Wasichoweza unaendeshwa na asasi ya T-MARC Tanzania kwa ufadhili wa watu wa Marekani kupitia Shirika la Maendeleo la Kimarekani USAID kwa ushirikiano na Vodacom Foundation.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo kwa wasichana walengwa wa mradi huu, Meneja wa Mradi wa Hakuna Wasichoweza, Bi. Doris Chalambo alisisitiza umuhimu wa kuwawezesha wasichana kama njia ya uhakika ya kufanikisha maendeleo ya  jamii na Taifa. ‘’Awamu ya kwanza ya mradi huu imewafikiwa jumla ya wasichana 5000 katika shule za msingi za Mtwara na jumla ya wasichana 1000 walioko nje ya shule katika kata 17. Walengwa wa mradi huu ni wasichana wenye umri wa miaka 9 – 15. Jumla ya shule 24 zimefikiwa na mradi huu ambao pia umetoa mafunzo kwa walimu 40 wa shule na Wakunga wa jadi, makungwi/Nyakanga 34 wanaotoa elimu kwa wasichana wanaobalehe’’.

Aliongeza kuwa lengo kuu la mradi wa Hakuna Wasichoweza ni kukuza viwango vya elimu kwa wasichana Tanzania kwa kuongeza mahudhurio yao shuleni. Lengo hili linafikiwa kwa kutoa msaada wa vifaa vya  kujisitiri katika kipindi cha hedhi kwa wasichana wa shule na walio nje ya shule wanaobalehe, pamoja na kutoa elimu ya afya na kujitambua itakayowasaidia wasichana kuepuka vishawishi vinavyosababisha utoro shuleni na mimba za utotoni.

Pia alisisitiza kwamba elimu hii juu ya masuala ya hedhi itawezesha kuongeza uelewa wa jamii kwa ujumla juu ya umuhimu wa kuwasaidia wasichana ili waweze kuhudhuria masomo yao kwa ufanisi zaidi na kufikia malengo yao kimaisha.

“Asilimia kubwa ya wasichana hutumia njia za asili ili kujisitiri wakati wa hedhi. Mara nyingi njia hizi si salama kiafya na ni chanzo cha magonjwa mbalimbali. Ningependa kutoa wito kwa jamii kwa ujumla kuvunja ukimya juu ya masuala ya hedhi kwani ni kwa uda mrefu kumekuwepo na imani potofu juu ya utumiaji wa vifaa vya kisasa vya kujisitiri wakati wa hedhi” Alimalizia Bi. Doris

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Vodacom Foundation,Yessaya Mwakifulefule alisema kuwa elimu inayotolewa na mradi wa Hakuna Wasichoweza italiwezesha Taifa kupunguza kasi ya maambukizi ya mgonjwa ya ngono ikiwemo VVU/UKIMWI miongoni mwa vijana. Akizungumza katika makabidhiano hayo, Mwakifulefule amesema kuwa kila msichana atakuwa akipatiwa pakiti mbili za vifaa hivyo kwa mwezi na zoezi hili litafanyika kwa muda wa miezi mitano mfululizo.

“Tunajivunia kuwa sehemu ya chachu ya maendeleo katika sekta ya elimu hususani mradi huu wa Hakuna Wasichoweza ambao umelenga kunufaisha jumla ya wasichana 6000 waliopo na wasiopo shuleni”.

Naye Mtaalamu wa Masuala ya Misaada kwa jamii kutoka Vodafone, Bi Laura Turkington alisema kuwa mradi unakuza ushiriki wa wadau mbali mbali katika kukuza viwango vya elimu pamoja na kutoa taarifa sahihi kwa jamii kuhusu changamoto zinazowakabili wasichana katika kipindi cha balehe.

T-MARC inatoa shukurani zake kwa shirika la USAID ambalo limetoa msaada wa dola za Kimarekani laki mbili (200,000)  kufadhili uanzishwaji wa mradi huu pamoja na Vodacom Foundation ambayo imechangia shilingi (TZS) 160 milioni kufanikisha awamu hii ya kwanza ya mradi.

No comments:

Post a Comment