Jeshi la Polisi Kanda Maalum
D’Salaam limefanikiwa kumbaini mtuhumiwa mhimu ambaye ni kinara wa mtandao wa
wizi katika mabenki ambaye anajulikana kwa jina la RONALD S/O MOLLEL umri miaka
37, mfanyabishara na mkazi wa Kimara Bonyokwa Jijini D’salaam.
Mtuhumiwa huyu amekimbilia
mafichoni mara baada ya tukio la ujambazi katika Tawi la Benki ya Barclays Kinondoni lililotokea tarehe 15/4/2014 ambapo
majambazi walifanikiwa kupora kiasi kikubwa cha fedha T.Shs.390,220,000/= , USD 55,000/= na EURO 2150/=. Aidha sasa imefahamika kwamba mtuhumiwa huyu
ni mume wa mtuhumiwa wa kwanza katika tukio la Barclays Benki aitwaye ALUNE D/O
KASILILIKA @ ALUNE D/O MOLLEL , miaka 28,
Mkazi wa Kimara Bonyokwa ambaye ni Meneja wa Benki Tawi la Barclays
Kinondoni. Mtuhumiwa Mollel anatafutwa
kwa kila hali kwa vile yeye ndiye alikuwa kinara wa kupanga tukio hilo la Barclays
na mara baada ya tukio ametoroka na kiasi kikubwa cha fedha hizo zilizoibiwa.
Zipo taarifa za kuaminika
kuwa mtuhumiwa huyu amekuwa akipanga na kushiriki kikamilifu katika matukio
mbali mbali ya uhalifu mkubwa ikiwa ni pamoja na kuongoza vikundi vya majambazi
vilivyowahi kupora katika mabenki mbali mbali katika kipindi cha mwaka mmoja
uliopita. Mtuhumiwa huyo ni hatari kwani
ana mtandao na watumishi muhimu katika matawi mbali mbali ya mabenki kwa lengo
la kufanikisha uhalifu katika mabenki hayo.
Jeshi la Polisi limelazimika
kutoa picha yake hadharani kwa kutumia dhana ya ulinzi shirikishi ili mtuhumiwa
huyu akionekana akamatwe na taarifa zitolewe katika kituo chochote cha Polisi
ikiwa ni lengo la polisi kupambana na uhalifu katika dhamira ya kuzuia uhalifu,
kulinda maisha na mali za wananchi.
Zawadi nono ya fedha taslim itatolewa kwa siri kwa mtu yeyote atakayetoa
taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa mtuhumiwa huyu. Pamoja na maelezo hayo mtuhumiwa mwenyewe
sasa anapewa fulsa ya kujisalimisha katika kituo chochote cha polisi kabla ya
kukamatwa kwa njia nyingine.
No comments:
Post a Comment