CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO; JIMBO LA KIGOMA KASKAZINI
TAMKO KUHUSU KUONDOKA KWA WALIOKUWA VIONGOZI
Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Kigoma Kaskazini
tunapenda kutoa taarifa kwa umma kutokana na sintofahamu inayotaka
kulazimishwa mbele ya jamii kuhusu uimara wa chama chetu mkoani Kigoma.
Tangu
jana na leo kumeenea taarifa zinazowahusu watu watatu, Jaffari
Kasisiko, Msafiri Wamarwa na Mama Malunga Masoud, ambao vyombo
mbalimbali vya habari vimeandika kuwa wamehama chama chetu cha CHADEMA
na kukimbilia wanakojua wao (maana CCM inafanya kazi zake katika sura
mbalimbali).
Katika hatua ya awali, sisi CHADEMA Jimbo la Kigoma Kaskazini tungependa kusema machache juu suala hilo la watu hao kuhama;
1. Kwanza
watu hao mbali ya kwamba walikuwa ni viongozi wa chama ngazi ya mkoa,
kwa uhakika kabisa walikuwa ni kikwazo kama si kizuizi cha muda mrefu
sana kwa chama chetu kustawi na kuwa imara zaidi katika mkoa mzima wa
Kigoma ili kiweze kukimbizana na wenzetu wa maeneo mengine nchi nzima.
Badala yake walikikumbatia na kukiatamia chama. Wakati maeneo mengine
wenzetu wakiongeza wabunge majimboni, Kigoma chini ya uongozi wao ikauza
majimbo.
2. Tunaweza
kusema kuwa viongozi hawa pamoja na wengine wachache ambao tunajua wako
mbioni kuondoka kati ya leo na kesho, walikuwa ni sawa na KOTI
LILILOTUBANA. Kwa muda wao wote wa uongozi hawakuwahi kufanya kazi
yoyote ya kioganazesheni na kukieneza chama mkoa mzima. Wao walikuwa
watu wa mikutano ya hapa na pale Kigoma mjini pekee au pale ambapo
kunakuwa na uongozi wa kitaifa au wabunge.
3. Kwa
muda mrefu saa wamekuwa viongozi ‘waliotubana’ kwa sababu walifanya
kazi kwa kuangalia zaidi maslahi yao. Sasa kuondoka kwao, ni nafuu kwa
chama. Pia ni fursa iliyokuja kwa wakati mwafaka kwa wanachama makamanda
waaminifu na watiifu waliofungiwa milango kwa muda mrefu, kusonga mbele
kukijenga chama chetu kwa imani kubwa ya kuendelea kubeba matumaini ya
Watanzania wanyonge.
4. Upo
ushahidi wa wazi katika hili. Kwa muda mrefu sasa viongozi hao na
wengine wenzao waliopangwa kuondoka kwa awamu nyingine, wamekuwa
wakilalamikiwa kufanya kazi ya chama kingine cha siasa kwa maslahi na
maelekezo ya CCM.
5. Katika
madai yao ya kuhama chama watu hao wamesema wamefikia hatua hiyo eti
kutokana na chama chetu kuwa cha kibabe eti kwa sababu tu Zitto Kabwe
alivuliwa nafasi Naibu Katibu Mkuu ndani ya chama!
6. Madai
hayo yanashangaza kwa sababu mbali ya chama kuwa na sababu nzito za
kumvua Zitto (na wenzake akina Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba) cheo
hicho kutokana na tuhuma za utovu wa nidhamu, pia tunaamini hakuna
mwanaCHADEMA amejiunga na chama hiki kwa ajili ya cheo. Ndani ya chama
chetu tunaamini katika kugawana majukumu si vyeo.
7. Katika
hali ya kushangaza zaidi wanasema eti Zitto amezuiwa kugombea
uenyekiti. Sasa tunajiuliza hiyo nia ya kugombea ambayo hatujawahi
kuisikia ikitangazwa kwa kufuata katiba, kanuni, maadili, miongozo na
itifaki za chama, waliambizana wao wenyewe na mtu wao? Lakini kwa
wanachama wa CHADEMA Mkoa wa Kigoma tunaelewa Jafari Kasisiko analipa
fadhila za misaada binafsi ikiwemo kupelekwa nje ya nchi.
8. Ninaomba
kutoa wito kwa viongozi wenzangu wa wilaya na majimbo ya Kasulu
Mashariki, Muhambwe, Buyungu, Kasulu Magharibi, Manyovu, Kigoma
Kaskazini, Kigoma Kusini na Kigoma Mjini, tukutane kwa ajili ya kikao
cha Baraza la Mashauriano la Mkoa ili sasa tuchukue hatua zingine za
muhimu na haraka za kuhakikisha tunasafisha chama chetu kwa kuwaondoa
vibaraka na wasaliti wote waliosalia.
9. Pia
tunaomba katika hali ya dharura Chama Makao Makuu pia kiingilie kwa
kutumia kifungu cha Katiba 6.1.3, ili kupata chombo cha kuendelea
kuwaunganisha wanachama wakati mkoa ukijiandaa kuchukua hatua hiyo
kupitia Baraza la Mashauriano.
10. Sisi
wa CHADEMA Kigoma Kaskazini tunawataka wale wengine waliosalia katika
mkakati huo wa kuhamisha watu wachache lakini kwa makundi ili eti
kujenga taswira ya CHADEMA kubomoka, wakiwemo viongozi kadhaa wa Kanda
wasisubiri. Chama chetu kitajengwa na watu wenye imani watakaoweka
maslahi na matakwa ya wananchi mbele kwa kuzingatia misingi yetu kama
inavyoelezwa katika Katiba ya Chama, kanuni, maadili na miongozo.
Kwa
niaba ya Wanachadema imara na makamanda watiifu na waaminifu kwa
mabadiliko yanayobeba matumaini na haki za Watanzania wanyonge, naomba
kutoa taarifa hii.
Ally Kisala
Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Kigoma Kaskazini
Mjumbe wa Baraza la Mashauriano la Mkoa wa Kigoma
No comments:
Post a Comment