Tuesday, July 15, 2014

Wapinzani walaumu undumilakuwili uchaguzi serikali za mitaa


Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba
Viongozi wakuu wa vyama vya siasa wamesema wamekuwa wakikanganywa kuhusu kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa kutokana na serikali kuwa na kauli mbili zisizoeleweka kuhusiana na uchaguzi huo.

Walisema hayo walipozungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana baada ya kuhudhuria mkutano wa kujadili masuala yanayohusu uchaguzi wa serikali za mitaa.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema hawafahamu hatma ya uchaguzi huo kutokana na kauli za serikali kwamba, mara inasema wanarekebisha katiba na hapo hapo wanaendeleza michakato ya uchaguzi.

Alisema serikali imekuwa ikiendelea na mchakato wa uchaguzi huo bila kuboresha kwanza sheria yake ili iendane na wakati kama walivyokubaliana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

 “Nje wanasema tunasubiri katiba mpya, ndani wanaendelea na michakato ya uchaguzi. Sasa hapo tuwaeleweje?” alihoji Profesa Lipumba.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika alisema mchakato unaoendelea juu ya maandalizi ya uchaguzi huo hauko sahihi.

Alisema wanachojua ni mabadiliko ya katiba kwenye sheria ya uchaguzi wa ngazi za mitaa kama walivyoahidiana na Pinda kuwa watarejea tena bungeni kujadili mchakato juu ya uchaguzi huo na kuboresha baadhi ya sera ili kuwa na uchaguzi huru na wa haki.

“Uchaguzi huu ufanyike kwa katiba yoyote, lakini kabla itungwe sheria mpya itakayoweza kuendesha shughuli hizo za uchaguzi. Na kauli za Rais, Waziri Mkuu na Waziri wa Tamisemi zisifuatwe kabla ya kutungwa kwa sheria hiyo,” alisema Mnyika.

Katibu wa Halmashauri Kuu (Nec), Mohamed Seif Khatib, aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kuitumia vyema nafasi waliyopewa ya mkutano wa kujadili masuala hayo kwa siku mbili ili watoe maoni yao.

Alisema wadau lazima waridhike na taratibu za kuendesha uchaguzi kwa sababu kuna maoni mengi wanatakiwa kuyasikiliza na wao kutoa yao.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro, Innocent Karogelis, alisema serikali ina wajibu wa kutimiza majukumu yake, kwani michakato ya mikutano hiyo ipo kwenye utaratibu wa kiserikali na lazima ifuatwe.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia alisema licha ya hoja iliyopo ya uchaguzi wa viongozi ngazi za msingi za serikali za mitaa usimamiwe na tume huru ya uchaguzi, ipo minong’ono kuwa wakurugenzi wa halmashauri wanatii Tamisemi kwa kuwa ndiyo inayowateua.

Hata hivyo, alisema uteuzi huo sio wa kisiasa, bali hufanywa kwa misingi ya stahiki kwa kuzingatia uwezo na taaluma kulingana na sera ya menejimenti ya utumishi wa umma na siyo kwa misingi inayozingatia matakwa ya mtu.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment