Jeshi la Polisi
Kanda Maalum linafanya uchunguzi kuhusiana na tukio la kukatika kiganja
cha mkono wa kulia cha mwanamke mmoja ajulikanaye kwa jina la MWANAHARUSI
D/O HAMISI, Miaka 43, mama wa nyumbani, Mkazi wa Mbagala Rangitatu.
Awali, Polisi walipokea
taarifa kuwa maeneo ya Mbagala Rangitatu Kibendera kijana mmoja CHARLES
S/O HUSSEIN MADOE, Miaka 26, Mkazi wa Mbagala Kombora anayetuhumiwa
kuiba pikipiki yenye namba za usajili T800 CTP aina ya Boxer rangi nyeusi,
anataka kuuawa na wananchi wenye hasira baa ya kuingia kwenye nyumba
ya mzee KALYA ili asiuawe.
Mara moja Polisi walifika
eneo la tukio ili kumwokoa kijana huyo ambapo walikuta wananchi wakiwa
wamezingira nyumba ya mzee huyo ambapo walitaka kuichoma moto ili mwizi
huyo afie ndani endapo hawatamtoa nje. Polisi walifanya kazi ya ziada
ili kumchomoa kijana huyo kwani wananchi walikuwa wanatupa mawe hovyo
na jiwe mja lilimpata askari G.6129 D/C TWALIB na kumjeruhi begani.
Iliwalazimu askari kutumia
mabomu ya machozi ili kuwatawanya wananchi na kujiokoa wao pamoja na
mtuhumiwa na ndipo walipofanikiwa kuondoka eneo la tukio. Baada ya hapo
zilipatikana taarifa kuwa katika nyumba ya jirani na eneo la tukio kuna
mwanamke mmoja amekatwa kiganja cha mkono wa kulia na bomu.
Kufuatia taarifa hizo
Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi ili kubaini chanzo halisi cha tukio
hilo na askari waliohusika katika tukio hilo wanahojiwa. Taarifa kamili
itatolewa baada ya uchunguzi kukamilika.
S. H. KOVA,
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM
No comments:
Post a Comment