WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali itaendelea kuyalinda makabila
madogo nchini yakiwemo ya Wahdazabe na Wasandawe ambayo yanategemea
rasilmali misitu kwa maisha yao na ustawi wao.
“Tutakuwa
tunafanya makosa kama tutawanyang’anya rasilmali misitu makabila madogo
hapa nchini kama vile Wahadzabe, Wandorobo na Wasandawe kwani ndiyo
rasilami pekee inayowawezesha wapate chakula cha kutosha,” alisema.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Novemba 11, 2014) wakati akifungua
Kongamano la Kwanza la Ufugaji Nyuki Barani Afrika la Mwaka 2014
lililoanza leo kwenye ukumbi wa AICC, jijini Arusha. Kongamano hilo
linashirikisha wajumbe 590 kutoka ndani na nje ya nchi. Nchi za nje
zinazoshiriki kongamano hilo ni 24, ambapo kati ya nchi hizo nchi 12 ni
za bara la Afrika.
Kongamano
hilo la siku tatu limeandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa
lengo la kuwakutanisha wafugaji nyuki, wafanyabiashara, wataalamu na
wawakilishi wa taasisi za ndani na nje ya nchi ili kujadili njia za
kuboresha ufugaji nyuki na kukabiliana na changamoto za ufugaji nyuki
hapa nchini na barani Afrika kwa ujumla.
Waziri
Mkuu aliwataka viongozi wa Halmashauri na watu wenye maamuzi
wasiwasumbue kwa kuwalazimisha wabadili maisha yao na kutoka kwenye
mfumo wa ikolojia (ecosystem) ambao wameuzoea. “Tusiwabugudhi, tusiwatoe
kwenye mfumo wao wa ikolojia. Tuwasaidie kuwapa teknolojia mpya ili
waweze kufuga kisasa na kupata faida huku wakiishi kwenye mazingira
hayohayo waliyoyazoea mpaka hapo watakapozoea na kuamua kubadilika kwa
kubaini kuwa njia zao za zamani haziwasaidii sana.”
Akizungumzia
kuhusu ufugaji nyuki barani Afrika, Waziri Mkuu alisema ufugaji nyuki
umeegemea zaidi katika rasilimali misitu na kilimo ambapo Afrika kwa
asilimia kubwa shughuli ya ufugaji nyuki hufanyika katika misitu.
“Bara
la Afrika lina ukubwa wa eneo la kilometa za mraba milioni 30.2 na
asilimia 20 ya eneo hilo ni misitu. Asilimia 40 ni misitu ya Savanna
ambayo ni muhimu kwa ajili ya ufugaji nyuki. Mapori haya pamoja na
maeneo ya kilimo yana uwezo mkubwa wa kuzalisha mazao ya nyuki kwa
wingi,” alisema Waziri Mkuu.
Akizungumzia
kuhusu ufugaji nyuki nchini Tanzania, Waziri Mkuu alisema takwimu za
Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) zinaonesha kuwa Tanzania ni
nchi ya pili barani Afrika inayozalisha asali kwa wingi (tani 34,000
kwa mwaka), ya kwanza ikiwa ni Ethiopia (tani 45,000 kwa mwaka).
“Inakadiriwa
kuwa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha tani 140,000 za asali na tani
10,000 za nta kwa mwaka. Lakini ni asilimia saba tu ya uwezo huo ndio
huzalishwa. Hii ni kwa sababu zao hilo limepuuzwa tangu siku nyingi na
halijapewa msukumo unaostahili.”
Alisema
sekta ya ufugaji nyuki ina mchango mkubwa katika maisha ya mwanadamu
kwa kumpatia chakula, ajira na kipato. “Wananchi hunufaika kutokana na
mauzo ya asali, nta na mazao mengine ya nyuki, utengenezaji wa vifaa vya
ufugaji nyuki, kusambaza malighafi za viwandani na huduma ya
uchavushaji,” aliongeza.
“Wafugaji
wa nyuki katika nchi zilizoendelea wanatumia teknolojia ya kuvuna sumu
ya nyuki (bee venom), gundi ya nyuki (propolis), maziwa ya nyuki (royal
jely) na chavua (pollen) ambavyo hutumiwa kama virutubisho na dawa.
Tafiti zimethibitisha kuwa gundi ya nyuki hutibu maumivu ya meno,
malaria na homa ya mifupa(arthritis) na kuongeza kinga mwilini. Sumu ya
nyuki imekuwa ikitumiwa kuongeza nguvu za uzazi, kutibu uvimbe na homa
ya mifupa,” alisema huku akishangiliwa.
Waziri
Mkuu aliitaka sekta binafsi na taasisi za utafiti barani Afrika
zifanye tafiti zaidi katika eneo hili na kuwekeza katika teknolojia
ambayo inaweza kuvuna na kuchakata mazao hayo ambayo yana soko kubwa
katika viwanda vya kutengeneza madawa, virutubisho na vipodozi.
Mapema,
akielezea kuhusu kongamano hilo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw.
Lazaro Nyalandu alisema Juni mwaka jana, Wizara hiyo ilisaini
makubaliano na Shirikisho la Ufugaji Nyuki Duniani (Apimondia) ili
waweze kuandaa kongamano la ufugaji nyuki barani Afrika mwaka 2014.
Alisema
kongamano hilo ambalo kaulimbiu yake ni: “Kufuga nyuki kwa kuzingatia
hifadhi ya mazingira na kukuza uchumi” yaani “African Bees for a Green
and Golden Economy” litahusisha mada 88 ambazo kati yake, 45
zitawasilishwa na watafiti wa kisayansi, 26 zitakuwa za majadiliano
(roundtable) na 17 zitawasilishwa katika semina.
Alisema
kongamano hilo ni kwanza kwa sababu ni mara ya kwanza kwa kongamano
kama kuandaliwa barani Afrika kwa kushirikiana na Apimondia kwa lengo la
kubadilishana uzoefu kuhusu species za nyuki zilizopo Afrika na
mazingira ya ufugaji nyuko barani humu.
No comments:
Post a Comment