Na Shamimu Nyaki-WHUSM
“Mkataa
kwao ni mtumwa”ni msemo ambao una maana kwamba binadamu ni lazima
ujikubali katika kila hali ambayo unakutana nayo katika mazingira yoyote
yale na usikubali binaadamu mwingine akakutawala au akabadilisha
mtazamo wako kwa manufaa yake bali kubali kupokea mawazo yanayoweza
kuboresha kile unachokiamini.
Na ndivyo alivyofanya
Baba wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kutumia
Kiswahili kama utambulisho wa Mtanzania popote pale atakapokuwa.
Katika Historia Lugha ya Kiswahili ilianza takriban miaka 800-1000 iliyopita katika
mazingira ya Vituo vya Biashara Ukanda wa Pwani ambako Wafanyabiashara
kutoka Uarabuni, Uajemi na Uhindi walikutana na wenyeji Waafrika.
Lugha kuu ya Kimataifa ya Biashara wakati huo ikiwa ni Kiarabu ambapo kutokana
na muingiliano wa watu lugha mpya ilijitokeza wakati wenyeji wa Pwani
waliokuwa wasemaji wa Lugha za Kibantu walipopokea maneno mengi hasa ya
Kiarabu katika mawasiliano yao.
Kiswahili kilikuwa na lahaja nyingi kutokana na lugha mbalimbali za Kibantu zilizochangia matumizi tangu Karne ya 19 ambapo Kiswahili kilianza kuenea Barani Afrika kwa njia ya Biashara.
Ni katika kipindi hiki ambapo Mwalimu Nyerere alikuwa katika harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika ndipo alipoamua kutumia lugha ya Kiswahili kama chombo muhimu cha kuwaunganisha Watanzania wote kupigania na kudai Uhuru.
Mara baada ya Uhuru mwaka 1961, Kiswahili kilitangazwa kuwa Lugha ya Taifa. Ambapo Waziri Mkuu wa kwanza wakati ule aliagiza kuwa Kiswahili kitumike katika shughuli zote za Umma.
Na katika kutekeleza Agizo hilo, tarehe 10 Desemba 1962, Rais wa Tanganyika wakati huo akiwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitoa Hotuba ya Jamhuri kwa Lugha ya Kiswahili. Katika
utetezi huo, hatua ya kwanza ya Mwalimu Nyerere ilikuwa ni usisitizaji
wa matumizi ya Kiswahili kama lugha asilia ambayo raia wa Tanganyika
walipaswa kutumia ili kuelewana ifaavyo, na kuondoa uwezekano wowote wa
mafarakano yanayohusiana na mitafaruku ya kimatamshi.
Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere akiwa na aliyekuwa Kiongozi wa China, Mwenyekiti Mao Tsetung.
Na
kwa kuweka mfano wa hatua hiyo, Rais Nyerere alihutubia katika hafla
zote rasmi kwa lugha ya Kiswahili, hivyo basi kuhakikisha kuwa kila raia
wa Tanganyika; aliyekuwa na kisomo au la; alimwelewa, pamoja na
mikakati ambayo Serikali yake ilipaswa kuweka.
La
kutia moyo ni kuwa,karibu asilimia 95 ya wakazi asilia wa Tanganyika,
ni wenye asili ya Kibantu, hivyo mazingira ya usisitizaji wa uzingatiaji
wa Kiswahili kuwa lugha unganishi ya jamii hizo yalifaa.
Hatua
ya pili kwa Rais Nyerere ilikuwa ni upitishaji wa Azimio la Arusha la
1967, aliposema kuwa, “ni mfumo wa 'Ujamaa’ pekee ambao ungefikia lengo
kuu la uuganishaji wa Watanzania wote”.
Katika
hotuba yake, kiongozi huyo alisisitiza kuwa, ni kupitia kwa Ujamaa
pekee, ambapo Waafrika wangeweza kupambana na falsafa kandamizi za
kibepari, akiurejelea mfumo wa ujima, ambao unawiana moja kwa moja na
ujamaa endelevu.
Mwalimu
Nyerere pia alikwepa matumizi ya falsafa ya kikomunisti, hasa kutoka
mataifa ya Urusi na Uchina, kwani yalihusishwa na ukandamizaji wa haki
za binadamu.Badala yake, alisisitiza mfumo wa demokrasia asilia,
uliotambua ushiriki wa kila mwanakijijji bila shaka, mafanikio ya ujamaa
yaliendelea kujitokeza kwani kadri vijiji hivyo vilivyoendelea kukua,
kiwango cha elimu kiliendelea kuimarika nchini Tanzania.
Kwa
mfano, kwa wakati mmoja, Tanzania iliorodheshwa nchi iliyokuwa na
kiwango kikubwa cha kisomo barani Afrika (asilimia 83) pamoja na
mafanikio makubwa katika sekta ya afya.
Hili
liliashiria kuwa, hakujikita pekee katika uongozi wa kisiasa, lakini
katika utetezi wa Kiswahili, kwani baadhi ya vitabu vyake aliviandika kwa Kiswahili ili kuwafaa wananchi na kuwafungua macho Watanzania kuhusu ilikokuwa ikielekea nchi yao.
Kutokana
na mchango huo, ni wajibu wa viongozi wetu wa kisiasa kutambua kwamba
mchango wao katika kuitetea lugha ndiyo utakaowafanya kukumbukwa na
vizazi vijavyo.
Uzalendo
wa Mwalimu Nyerere unapaswa kuwa mwanga kwa viongozi wote wa Kiafrika
kufahamu kwamba kutumia Kiswahili ni wino wa kuandika historia.
Mwalimu Nyerere atakumbukwa kwa kuwa miongoni mwa Waafrika wa kwanza kutafsiri kazi za Kiingereza kwa Kiswahili.
Mwalimu J. K. Nyerere akiwa na Rais wa Kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela
Juhudi hizo zimeendelea kuonekana kwani Januari
1967 Agizo jingine lilitolewa na Makamu wa Pili wa Rais wakati huo
Mheshimiwa Rashidi Mfaume Kawawa kwamba, Kiswahili kitumike katika
shughuli zote za Kiserikali na Kitaifa.
Kuanzia hapo Kiswahili kikawa kinatumika katika shughuli zote za Nyanja zote hapa nchini na kimeimarisha mahusiano ya makabila na kuifanya Nchi ionekane kama ina kabila moja
badala ya makabila takriban 120. Kiswahili kimekuwa Nguzo Imara ya
Mshikamano, Amani, Utulivu na Upendo miongoni mwa Watanzania.
Ama
kwa hakika juhudi hizi zimezaa matunda kwa Watanzania kutokana na umoja
uliotakana na juhudi za mwalimu katika kueneza matumizi ya lugha yetu
na ni kutokana na juhudi za viongozi wote wa nchi hii wanavyohimiza kutumia lugha hii.
Kudhihirisha hilo Rais wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Kikwete katika hotuba yake kwanza aliyoitoa Bungeni baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Disemba 2005 alisema “Lugha ya Kiswahili imeanza kupata umaarufu Afrika na duniani”.
Umoja wa Afrika umekubali Kiswahili kuwa moja ya lugha zake kuu. Aidha Nchi za Kanda ya Maziwa Makuu zimekubali kutumia na kuendeleza lugha ya Kiswahili.
“Serikali
ya Awamu ya Nne itahakikisha kuwa juhudi hizi zinaendelezwa na
kuhakikisha kuwa lugha ya Kiswahili inakua nje ya mipaka ya
Afrika”.Alisema Mhe. Kikwete.
Hizi
ni jitahada kubwa sana zilizofanywa na ambazo zinaendelea kufanywa na
Serikali katika kuhakikisha lugha ya Kiswahili inakuwa kwa kiasi
kikubwa.
Kipo
chombo Muhimu kilichopewa dhamana ya kuendeleza na kukuza lugha hii kwa
ubora zaidi ambacho ni Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ambalo lipo chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
liliundwa chini ya sheria namba 27 ya Bunge ya mwaka 1967 kukuza na
kuendeleza matumizi ya Lugha ya Kiswahili katika Tanzania,kushirikiana
na taasisi nyingine ndani ya Jamhuri ya Muungano ambazo zinahusika na
kukuza Kiswahili na kuratibu kazi zao,kukuhamasisha matumizi ya Lugha ya
Kiswahili katika shughuli rasmi na za umma.
Mafanikio
haya ya matumizi ya Kiswahili yamesaidia sana kukuza na kuendeleza
lugha ya Kiswahili kwani Hata Rais wa Awamu ya Tano Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli yupo mstari wa mbele katika kutumia lugha hii ya Kiswahili
katika hotuba zake na dhifa mbalimbali za Kitaifa Mfano ni wakati
alipokutana na Waziri Mkuu wa India Mhe.Narendra Modi tarehe 29 mwezi
Agosti 2016.
Watanzania
wote tunapaswa kujivunia juhudi hizi na tuwe mstari wa mbele kuendelea
kukitumia Kiswahili kama utambulisho wetu ili kueneza utamaduni wa nchi
yetu.
No comments:
Post a Comment