Mtandao wa wadau kutoka asasi za kiraia unaotetea marekebisho ya sheria na sera ihusuyo usalama
barabarani Tanzania siku ya tarehe 26 na 27 Januari, 2017 wamefanikiwa kukaa na baadhi ya wabunge
kutoka kamati ya mambo ya nje, Ulinzi na usalama, Katiba na sheria pamoja na miundo mbinu katika
kikao kilichoongozwa chini ya mwenyekiti wake Mbunge wa Muheza Mheshimiwa Balozi Adadi
Rajabu, pamoja walionyesha ushirikiano wao katika kuboresha usalama bararani kwa maendeleo ya
Taifa letu.
Wajumbe wa kikao husika walipata nafasi ya kusikiliza mada mbalimbali kuhusiana na masuala ya
usalama barabarani na hali ilivyo sasa, ambapo ilielezwa kuwa hali ilivyo kulingana na takwimu
zinaonyesha kuwa takribani watu milioni 1.25 hufariki dunia kila mwaka kutokana na ajali za barabarani,
aidha, watu milioni 20 hadi 50 hujeruhiwa na wengine hupata ulemavu wa kudumu wengi wao wakiwa ni
vijana wenye nguvu kazi ya Taifa. Hii ni kutokana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) 2015.
Kwa upande waTanzania Bara, taarifa kutoka jeshi la polisi Kikosi cha Usalama Barabarani inaonyesha
kwamba, kwa mwaka 2016 jumla ya watu 3,256 walipoteza maisha kutokana na ajali za barabarani.
Katika vifo hivyo wanaume ni 2,580 na wanawake ni 676. Aidha kumekuwa na majeruhi 8,958 kati
yao wanaume ni 6,470 na wanawake 2,488. Wakati vyombo vya moto vilivyoongoza katika ajali ni
magari binafsi ambayo idadi yake 3,649 ikifuatiwa na pikipiki kwa idadi ya 2,544.
Kutokana na idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani nchini, Mtandao wa wadau
kutoka asasi za kiraia unaotetea marekebisho ya sheria na sera zinazohusu usalama barabarani Tanzania
umeona umuhimu na kuchukulia jambo hili kulifanyia kazi kwa kina. Tafiti zinaonyesha kwamba
asilimia 76 ya ajali zote zinatokana na vyanzo vya kibinadamu kama vile Ulevi, Mwendokasi, Uzembe,
Uchovu, kupuuzia au kutokuwa makini uwapo barabarani na kutokutii sheria za Usalama Barabarani.
Tuna amini matendo haya ya kibinaadamu yana dhibitika kisheria, hivyo basi tunaisihi serikali
kuboresha sheria.
Kama wadau wa Usalama Barabarani, tunadhani kuna umuhimu wa sheria sasa kuboreshwa, na hivyo
utashi wa kisiasa unatakiwa. Ndiyo maana tukaitisha majadiliano ya pamoja na Wabunge pamoja na
wadau mbalimbali wa Usalama Barabarani ili kuona ni kwa namna gani tunaweza kuleta mabadiliko ya
sheria kwa ufanisi na kwa haraka.
Wabunge waliohudhuri kikao hiki kwa ujumla wao, waliona umuhimu wa kuwa na mikakati ya kitaifa
ya kupunguza ajali na walikiri kwa nia moja na kukubali kuunda Mtandao wa Wabunge wanaotetea
usalama barabarani.
Maeneo ambayo tunayapa kipaumbele katika maboresho ya sheria ni kama haya yafuatayo:
a) Matumizi ya mikanda; Sheria ya sasa ya Usalama barabarani inasema ni kosa kisheria kwa dereva
na abiria anayekaa kiti cha mbele kutokufunga mkanda wakati wa safari lakini sheria hiyo hiyo
haisemi chochote kwa abiria wanaokaa kiti cha nyuma.
Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) unasema kuwa iwapo ajali ikitokea
madhara/athari kwa abiria wa kiti cha mbele itapungua kwa 50% na kwa abiria wa nyuma madhara
yatapungua kwa 70%. Kanuni zilizotungwa na SUMATRA zinataka abiria wote wafunge mkanda ila
kwa vile sheria mama (Road Traffic Act of 1973) ipo kimya katika eneo hili utekelezaji wa kanuni
unakuwa mgumu.
Hivyo basi ni rai yetu sheria hiyo ibadilishwe na kuwataka abiria wote wanaokuwa katika chombo
cha usafiri wa kibiashara au binafsi kufunga mkanda wakati wote wa safari.
b) Matumizi sahihi ya kofia ngumu; Sheria ya sasa ya usalama barabarani inasema kuwa ni kosa kwa
muendesha pikipiki kutokuvaa kofia ngumu wakati wa kuendesha chombo hicho. Lakini sheria
hiyohiyo haisemi chochote kwa abiria anayepanda katika chombo hicho.
Vilevile pamoja na kuanisha kosa kwa dereva wa pikipiki kutokuvaa kofia ngumu lakini pia sheria
haielezi ni jinsi gani kofia inatakiwa kuvaliwa na aina maalum ya kofia inayotakiwa kuvaliwa.
Kwa mujibu wa Utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unaonyesha kuwa iwapo ajali itatokea
madhara yanayotokea kwa kutovaa kofia maalum na kwa usahihi ni makubwa sana ukilinganisha na
kofia hiyo ikivaliwa kwa usahihi. Hivyo basi ukizingatia kuwa sasa hivi usafiri wa pikipiki umekuwa
unatumika kwa kiasi kikubwa (public transport) hivyo ni rai yetu sheria hiyo ifanyiwe maboresho na
kuweka kuwa ni sheria kwa mtu yoyote anayepanda pikipiki kuvaa kofia ngumu na kwa usahihi.
c) Ulevi: Sheria ya sasa ya usalama barabarani inasema kuwa itakuwa kosa kwa mtu yoyote kuendesha
chombo cha moto akiwa na kiwango cha kilevi katika damu yake kinachozidi asilimia 0.08% katika
mfumo wa mwili. Kiwango hiki ni kikubwa sana kikilinganishwa na tafiti zilizofanywa na Shirika la
Afya Duniani na kupendekeza kiwango cha asilimia 0.05% kwa dereva aliyebobea (experienced
driver) na asilimia 0.02% kwa dereva mchanga (young driver). Hivyo basi ni rai yetu kuwa sheria
ifanyiwe marekebisho ili iendane na kiwango cha sasa cha kimataifa kilichofanyiwa utafiti.
d) Mwendo kasi (Speeding): Mwendokasi umeendelea kuwa sababu kubwa ya ajali zinazogharimu
uhai wa watu wengi. Sheria yetu inayo mapungufu kadhaa pamoja na juhudi nyingi za Jeshi la Polisi
na wadau wengine kutaka kudhibiti jambo hili limeendelea kuwa tatizo. Adhabu zisizokidhi wala
kuleta hofu kwa maderava wasiotaka kutii zimeendelea kufifisha juhudi za kudhibiti tatizo hili.
Tunatoa wito kwa watunga sera kushirikiana zaidi na wadau kuuelimisha umma katika eneo la
uhusiano wa adhabu zitokanazo na makosa ya usalama barabarani na ongezeko la ajali. Pia sheria
kufanyiwa maboresho na kuangalia kwa upya mianya iliyopo.
TAMKO HILI LIMETOLEWA LEO NA MTANDAO WA WADAU KUTOKA ASASI ZA KIRAIA:
1. TAWLA
2. TAMWA
3. WLAC
4. TCRF
5. TLS
6. TMF
7. RSA
8. AMEND TANZANIA
9. SHIVYAWATA
10. TABOA &
11. SAFE SPEED FOUNDATION
No comments:
Post a Comment