Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (kulia akisalimiana na
Balozi Mstaafu Msuya Waldi Mangachi aliyefika Ofisini kwake Baraza la
Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)
Balozi
Mstaafu Msuya Waldi Mangachi (kushoto), akimkabidhi Balozi Seif Ali
Iddi nakala ya kitabu alichokitunga kinachoelezea uzoefu wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki ya zamani kwenye mazungumzo yao. Balozi Mstaafu Msuya Waldi Mangachi (kushoto), akifafanua jambo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi. Wa kwanza kutoka kulia ni Msaidizi wa Balozi Mstaafu Msuya, Bwana Msangi Mangachi na aliyepo katikati ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Balozi
Seif Ali Iddi (kulia), akiwa makini kufuatilia ufafanuzi uliokuwa
ukitolewa na Balozi Mstaafu Msuya Waldi Mangachi wakati akielezea
yaliyomo ndani ya Kitabu alichotunga kinachoelezea uzoefu wa Jumuiya ya
Afrika Mahshariki ya zamani.
Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
15/2/2017.
MGAWANYO
wa fursa za uwekezaji unaofanywa na Kampuni na Taasisi za Kimataifa
ndani ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ukizingatiwa vyema kulingana na
ushiriki wa nchi wanachama utaiongezea dira na umadhubuti Jumuiya hiyo
katika malengo yake ya muda mrefu.
Kauli
hiyo imetolewa na Balozi Mstaafu wa Tanzania ambae kwa sasa amekuwa
mhadhiri wa Elimu ya Chuo Kikuu Nchini Balozi Msuya Waldi Mangachi
wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi katika Ofisi za Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa
Zanzibar.
Balozi
Msuya Waldi Mangachi ambae katika mazungumzo hayo alimkabidhi nakala ya
Kitabu alichokitunga kinachoelezea uzoefu wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki ya zamani alisema mgawanyo wa fursa hizo utakaokuwa na
muelekeo wa kutumia maeneo yote utasaidia kuondoa au kupunguza
malalamiko yanayoweza kuonyesha sura ya upendeleo wa upande mmoja.
Balozi
Msuya alisema sababu za msingi zilizopelekea kuvunjika kwa Jumuiya ya
Afrika ya Mashariki mnamo mwaka 1977 ilitokana na mitizamo tofauti ya
kisiasa na hasa falsafa ya kujenga uchumi baina ya Nchi wanachama wa
Jumuiya hiyo.
Mtaalamu
huyo wa Fani ya Udaktari wa Historia alieleza kwamba Jumuiya ya Afrika
ya Mashariki ya zamani isingeweza kufanikiwa bila ya kubadilika kwa
mfumo wa uchumi Kimataifa.
Alisema
mfumo uliotumika ulizikuta Nchini wanachama zikizalisha malighafi na
kuziuza kwa nchi za Kaskazini na matokeo yake wanunuzi hao walichakachua
malighafi hiyo na kuzirejesha kwa wazalishaji hao kama bidhaa za
Viwandani.
Balozi
Msuya alifafanua kwamba mantiki ya ushirikiano uliopo ndani ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki bado haijakaa vizuri licha ya kwamba biashara huru
ndio njia pekee ya kuimarisha ushirikiano wa Jumuiya yoyote ile iwe ya
Nchi au ya kanda.
Hata
hivyo Balozi Mstaafu Msuya Waldi Mangachi aliipongeza Jumuiya ya Afrika
Mashariki kwa utendaji wake uliopiga hatua ya ufanisi ikiwa bado mfano
mzuri kulinganishwa na Jumuiya nyengine zilizowahi kuundwa ndani ya Bara
la Afrika.
Alipendekeza Nchi Mwanachama kupewa haki na fursa ya mapato yake inayokusanya kwa mujibu wa uuzaji wa ulinganifu.
Akitoa
shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alimpongeza Balozi huyo Mstaafu ambae pia Mhadhiri wa Elimu ya Chuo
Kikuu Nchni Balozi Msuya Waldi Mangachi kwa uamuzi wake wa kuandika
Historia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Balozi
Seif alisema Historia ya Kitabu hicho itatoa fursa zaidi kwa Kizazi
kipya kuelewa malengo ya Waasisi wa chimbuko la Jumuiya hiyo waliokuwa
na muono mpana zaidi.
No comments:
Post a Comment