NA ESTOM SANGA- SHINYANGA
Walengwa
wa Mpango wa kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo
ya Jamii- TASAF mkoani Shinyanga wameeleza kunufaika na fedha
zinazotolewa na mfuko huo kama ruzuku kwa kuanzisha miradi midogo midogo
na hivyo kujiongezea kipato na kupunguza tatizo la umaskini lililokuwa
linawakabili kabla ya kuanza kwa Mpango huo.
Wakizungumza
na Waandishi wa Habari waliotembelea baadhi ya kaya za walengwa wa
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Manispaa ya Shinyanga baadhi ya
walengwa hao wameeleza kuwa wameweza kuanzisha miradi ya ufugaji wa
nguruwe, mbuzi, ng’ombe na kuku kwa kutumia ruzuku ya fedha walizozipata
kupitia utaratibu wa uhawilishaji fedha unaofanywa na TASAF.
Walengwa
hao wamesema kabla ya kuingizwa kwenye utaratibu wa Mpango wa Kunusuru
Kaya Maskini,walikuwa wakihangaika na kushindwa kupata fedha za
kuanzisha miradi midogo midogo kutokana na kutokuwa na fursa ya kupata
mikopo kutoka katika taasisi za fedha na hivyo kutopea katika dimbwi la
umaskini.
“Ninaishukuru
sana serikali kwa kutuletea TASAF kwani imetufungua macho na kuwa
chachu ya maendeleo kwani sasa naishi kwenye nyumba yangu niliyoijengwa
baada ya kudunduliza fedha kutoka TASAF” amesisitiza Bi.Christina
Ndimila (70) mkazi wa Ndala A katika manispaa ya Shjinyanga.
Walipoulizwa
wanawezaji kuanzisha miradi hiyo ilhali baadhi ya watu wanadai kuwa
ruzuku ya fedha inayotolewa na TASAF ni ndogo, walengwa hao wamesema
kuwa matumizi sahihi na kuzingatia masharti ya Mpango ndiyo
kumewawezesha kujiwekea akiba kidogo kidogo ya fedha hizo kila
wanapozipata.
“
Ukizipata fedha za TASAF na kuzila zote utaziona kuwa ni ndogo ,lakini
ukipata na kuziwekeza kwenye mradi wowote mdogo fedha hizo huongezeka
baada ya muda mfupi na hivyo kukupa uwezo wa kujiendeleza” alisisitiza
Bi. Joyce Jindai Lubunga(59) mmoja wa walengwa wa Mpango wa Kunusuru
Kaya maskini anayeishi katika mtaa wa Banduka nje kidogo ya manispaa ya
Shinyanga.
Waandishi
wa habari waliotembelea Baadhi ya walengwa katika manispaa ya Shinyanga
wameshuhudia baadhi yao wakitumia sehemu ya fedha za ruzuku kutoka
TASAF kuboresha makazi yao kwa kujenga nyumba, kuanzisha bustani za
mboga mboga hususani nyanya, ufugaji wa nguruwe, mbuzi, kuku na ng’ombe
shughuli ambazo zimeendelea kuwaongezea kipato.
Hata
hivyo mbali ya mafanikio hayo walengwa hao wameeleza kuwa wanakabiliwa
na tatizo la utaalamu wa mifugo hususani uwezo mdogo wa kukabiliana na
magonjwa yanayokumba mifugo yao na hivyo kuomba wataalamu wa mifugo
kuwatembelea kwenye maeneo yao na kuwapa ushauri wa namna ya kuboresha
shughuli zao ili waweze kupata mafanikio zaidi.
Zifuatazo
hapo chini ni baadhi ya picha za walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya
maskini katika manispaa ya Shinyanga wakionyesha mafanikio na miradi
wanayoitekeleza baada ya kupata ruzuku kutoka TASAF.
Mmoja
wa walengwa wa TASAF katika manispaa ya Shinyanga akiwa nje ya nyumba
yake aliyoijenga kwa fedha za ruzuku kutoka TASAF ikiwa ni jitihada za
kuboresha makazi yake na picha ya chini mlengwa huyo akiwaonyesha
Waandishi wa habari baadhi ya mbuzi aliowanunua kutokana na ruzuku hiyo.
Mmoja
wa walengwa wa TASAF bi. Maria Gabriel Picha ya juu akiwa karibu na
nyumba yake ya zamani na chini ni nyumba yake mpya aliyoijenga baada ya
kupata fedha za ruzuku kutoka TASAF.Picha inayofuatia ni bomba la maji
alilovuta kutokana na fedha za ruzuku hiyo.
Mmoja
wa walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya maskini Bi.Perpetua Tungu picha
ya chini akiwa katika bustani yake ya mboga aliyoianzisha kutokana na
fedha za ruzuku kutoka TASAF kama sehemu ya kujiongezea kipato. Picha ya
chini inaonyesha nyumba anayoendelea kuijenga kwa kutumia fedha hizo
ikiwa ni jitihada za kuboresha makazi yake.
Mmoja
wa walengwa wa TASAF BI. Rehema Naligigwa katika manispaa ya Shinyanga
akionyesha banda analolitumia kufuga nguruwe baada ya kupata fedha za
ruzuku kutoka TASAF.
No comments:
Post a Comment