Dar es Salaam. Taasisi ya mikopo ya Pride Tanzania ipo taabani kifedha ikidaiwa kushindwa kujiendesha.
Licha ya hilo, taasisi hiyo inadaiwa kuwa imeshindwa kutoa mikopo kwa wateja wake na kulipa stahili za wafanyakazi ikiwa pamoja na michango ya pensheni na kodi ya Serikali.
Pride ilianzishwa Mei 5, 1993 chini ya Sheria ya Kampuni (CAP 212) kwa lengo la kutoa mikopo midogomidogo kwa wajasiriamali. Hata hivyo, utendaji wake umekuwa ukishuka siku hadi siku.
Mkurugenzi mkuu wa Pride yenye makao makuu jijini Arusha, Rashid Malima alipoulizwa kwa simu kuhusu hali ya taasisi hiyo kifedha, alisita kuzungumza akisema ametingwa na mambo mengi.
Taarifa kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi wa makao makuu jijini Arusha zilisema tangu Desemba 2016, uongozi wa Pride umeshindwa kuwasilisha michango ya pensheni kwenye Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) inayofikia Sh1.8 bilioni jambo lililosababisha wafungue kesi.
“Huo ni ukweli mtupu, ndiyo maana tumefungua kesi, lakini kinachotukatisha tamaa ni kuona kesi hiyo imekuwa ikipigwa kalenda na inaweza kuahirishwa hata kwa miezi sita,” alisema mtoa taarifa ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini. Mbali na pensheni, mtoa taarifa huyo alidai kuwa Pride imeshindwa kupeleka kodi ya mishahara (Paye) kwa zaidi ya mwaka mmoja, huku pia ikishindwa kuhudumia wateja wake.
Mfanyakazi mwingine wa taasisi hiyo aliiambia Mwananchi kuwa kila tawi limeagizwa kupeleka makao makuu Sh40 milioni kila mwezi kama fedha za matumizi ya ofisi.
“Pamoja na matatizo yote ya kushindwa kutoa mikopo kwa wateja wetu, tunatakiwa kupeleka Sh40 milioni za obligation (lazima) kila mwezi,” alisema.
Mwandishi wetu alizungumza na wateja wa Pride Tanzania katika tawi la Kariakoo jijini Dar es Salaam waliothibitisha kuwapo kwa hali mbaya ya mikopo.
Khalfan Bakari, ambaye ni mteja wa tawi hilo alisema hali ya taasisi hiyo ilianza kuwa mbaya baada ya mwaka 2016 huku akihusisha na mikakati ya Serikali kutilia mkazo ukusanyaji wa kodi.
“Hali mbaya ilianza tangu utawala wa awamu hii ulipoanza mwaka 2016 kwa kudai kodi. Kwanza kulikuwa na utata wa umiliki wa Pride...,” alisema Bakari.
Akizungumzia madhara yaliyojitokeza kwao, alisema awali mtu akiomba mkopo anajadiliwa wiki ya kwanza na wiki ya pili anapewa, lakini kwa sasa inakwenda hadi miezi sita bila kupata.
“Kuna watu hapa hawajapata mikopo tangu walipoomba Juni mwaka huu. Wengine wamekata tamaa wamejitoa, lakini nao wameshindwa kupewa akiba zao,” alisema.
Christina Alex, ambaye pia ni mteja alisema alishamaliza deni na kujitoa uanachama, lakini hajapewa akiba yake aliyoichanga miaka sita iliyopita. “Hali ni mbaya sana Pride, zamani kila siku kuna makundi ya watu 50 waliokuwa wakihudumiwa kila baada ya saa moja tangu saa tatu asubuhi hadi saa 10 jioni, lakini siku hizi, watu wamepungua hadi 15 kwa saa moja na muda wa kuwahudumia umepunguzwa hadi saa 7:30 mchana,” alisema Christina.
Maelezo ya wateja hao yaliungwa mkono na ofisa mikopo wa Pride ambaye pia hakutaka jina lake litajwe gazetini, akisema hata ulipwaji wa mishahara umekuwa wa kusuasua. “Kimsingi hali mbaya, ila wamekuwa wakificha, kwa sababu hawawezi kuwaambia waziwazi wafanyakazi na wateja,” alisema na kuongeza:
“Siku hizi hata mishahara tunalipwa kwa kusuasua, hata baada ya miezi miwili na wakati mwingine tunalipwa kidogokidogo. Hata makato ya wafanyakazi wanaolipa mikopo ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB) haipelekwi siku hizi,” alisema mfanyakazi huyo.
Taarifa za kusuasua kwa Pride zimekuja huku pia kukiwa na utata wa umiliki wake kwani licha ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kusema siyo shirika la umma, Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) katika taarifa yake ya mwaka 2015/16 alihoji uhamishwaji wa hisa za Pride Tanzania kutoka serikalini kwenda kwa watu binafsi.
“Taarifa ya Msajili wa Hazina ilionyesha hisa zote za Pride zinamilikiwa na Serikali mpaka Juni 30, 2008. Hata hivyo, Juni 30, 2012, Pride iliondolewa kwenye orodha ya mashirika ya umma. Uhalali na sababu ya kuondolewa kwa Pride katika orodha ya mashirika ya umma haikubainika,” inasema taarifa ya CAG. Taarifa hiyo inataja kifungu cha 31 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na.11 ya mwaka 2008 kinachotaka kila shirika la umma kupeleka hesabu kwa CAG kukaguliwa katika kipindi cha miezi mitatu baada ya kumalizika kwa mwaka wa fedha.
“Hata hivyo, hesabu za Pride Tanzania hazijawahi kuwasilishwa kwenye ofisi yangu kama inavyotakiwa na sheria. Pamoja na majibu ya Serikali kuwa kampuni imeacha kupata fedha kutoka kwa Serikali ya Kifalme ya Norway na Tanzania mwaka 2005, haijawekwa wazi jinsi hisa za kampuni hii zilivyohamishwa kwenda kwa wamiliki binafsi,” alisema CAG.
“Hivyo basi, ninaendelea kusisitiza kuwa Msajili wa Hazina anapaswa kufuatilia kwa karibu juu ya umiliki wa kisheria wa hisa za Pride Tanzania zilizokuwa zinamilikiwa na Serikali na baadaye kuhamishiwa kwa wamiliki binafsi,” inaeleza taarifa ya CAG.
Taarifa ya CAG pia inataja deni la Pride Tanzania la Sh5.3 bilioni la mwaka 2014 ambalo ni mkopo uliotolewa na Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB).
“Hadi kufikia Desemba 2014, Pride ilikuwa ikidaiwa Sh5.3 bilioni ambao ni mkopo uliotolewa na Benki ya Uwekezaji (TIB),” inasema taarifa hiyo.
“Mkopo huo umedhaminiwa na wadaiwa wa Pride, ikimaanisha wakati kampuni ikishindwa kulipa madeni, madeni hayo yatalipwa kwa kutumiwa wadaiwa wa Pride. Dhamana ya aina hii haina uhakika na inaweza kusababishia benki hasara.”
CAG aliishauri menejimenti ya Pride kuongeza nguvu ili kuhakikisha mkopo huo unalipwa na kutoa mikopo kwa kwa wakopaji wenye dhamana ya kueleweka.
No comments:
Post a Comment