Friday, September 23, 2016

Misitu na mazingira vikisimamiwa ipasavyo vitaboresha maisha ya wananchi vijijini.


Dr. Nicole Cross-Camp ambaye ni Mtafiti kutoka Chuo kikuu cha East Anglia cha nchini Uingereza chini ya mradi wa ESPA (Ecosystem Services for Poverty Alleviation) akitoa mada kuhusiana na matokeo ya utafiti kuhusu changamoto wanazozipata wanakijiji katika utunzaji wa misitu kwa wadau kutoka Wizara mbalimbali pamoja na Sekta binafsi.
Maneja Mradi, Lasima Nzao akiwasilisha matokeo ya utafiti uliopo chini ya mradi wa ESPA (Ecosystem Services for Poverty Alleviation). Mkutano huo ulifanyika katika Hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam.

Wadau wa Mistu na Mazingira kutoka Serikalini, Taasisi na Mashirika binafsi walikutana na watafiti hao ili kujadili matokeo hayo ya utafiti na kuweza kuchanganua mbinu mbalimbali za kuweza kukabiliana na changamoto na faida zinazotokana na usimamizi wa misitu kwa wanajamii wanazozungukwa na hifadi ya misitu hapa Tanzania.

Akizungumza na Lasima Nzao na Dr Nicole Gross-Camp walisema kuwa utafiti huo uliofanyika katika vijiji nane vya wilaya mbili, halmashauri ya wilaya ya Iringa vijijini na wilaya ya Kilwa kuanzia Septemba 2014 na kumalizika september 2016 na ulikuwa "unaangalia mchango wa misitu inayosimamiwa na Jamii (CBFM) katika kuboresha hali ya maisha kwa wanakijiji husika". 

Utafiti unaonyesha  kuwa mistu na mazingira ikisimamiwa  ipasavyo inaweza kuboresha maisha ya wananchi walio vijijini kwa kuwa wanajamii wanapenda mfumo wa misitu ya jamii japokua bado kuna changamoto nyingi katika usimamizi wa misitu kwa wanajamii hasa misitu inayosimamiwa na Jamii.

Utafiti huo ulidhaminiwa na ESPA, UKAID, NERC na ESRC na ulifanywa na mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha East Anglia UEA nchini Uingereza Dr Nicole Gross-Camp akishirikiana na mtafiti kijana wa kitanzania, Lasima Nzao ambaye pia alikua meneja wa mradi wa Utafiti huo.
Mtafiti na Mshauri wa masuala ya Misitu, Kihana Lukumbuzya akichangia mada baada ya wataalamu kuwasilisha utafiti uliofanyika katika vijiji nane ndani ya wilaya mbili.
Mshauri wa masuala ya Misitu na Mabadiliko ya Tabianchi, Faustine Ninga akichangia mada kuhusu  utafiti uliofanyika katika wilaya mbili kuhusu mchango wa jamii (CBFM) katika kuboresha hali ya maishaya wanajamii.
 Gabriel Marite Ole Tuke
Msimamizi wa Maliasili kutoka Mkoani Dodoma, Sanford Kway akichangia mada
Picha ya pamoja

Prof Mbarawa ateua wajumbe Bodi ya Posta


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilino Prof Makame Mbarawa ameteuai wajumbe sita wa Bodi ya Shirika la Posta Tanzania.
Hatua hiyo inafuatia Rais Dk John Magufuli kumteua Luteni Kanali Mstaafu, Haroun Ramadhan Kondo kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya ya Shirika la Posta Tanzania hivi karibuni.
Taarifa ya Katibu Mkuu Wizara hiyo anayeshughulikia Mawasiliano, Prof Faustine Kamuzora imesema Prof Mbarawa ametangaza uteuzi huo leo kwa mujibu wa sheria za shirika la Posta Tanzania No 19 ya mwaka 1993 kifungu cha 1(b) na uteuzi huo ulianza tangu Septemba 5 mwaka huu.
Wajumbe walioteuliwa kusaidiana na Luteni Kanali Mstaafu Kondo na watadumu katika nyadhifa hizo kwa kipindi cha miaka mitatu ni pamoja na Mhadhiri wa sheria za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) na Mkuu wa Idara ya Mafunzo Chuo Kikuu Mzumbe, Dk Ubena John, Mchumi Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jasson Bagonza, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Benki ya TIB, Stella Nghambi.
Wajumbe wengine ni Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Inonovex, Leonard Kitoka, aliyekuwa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Posta Tanzania, Zanzibar, Fatma Juma Bakari na Mratibu Mkazi wa Misaada ya 

Taasisi zachangia mil 172/- maafa Kagera

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amepokea hundi za thamani ya Sh milioni 140, vifaa vya ujenzi na vyakula vya thamani ya Sh milioni 32.5 kwa ajili ya kuwachangia Watanzania waliopata maafa ya tetemeko la ardhi mkoani Kagera Septemba 10, mwaka huu.

Akipokea msaada huo, Majaliwa aliyashukuru makundi sita yaliyofika ofisini kwake kuwasilisha hundi hizo kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania hao na kusema huo ni mwendelezo wa walioguswa na jambo hilo kwa kuendelea kutoa kile walichonacho.
Alisema wote waliochangia michango hiyo ataiwasilisha kwa wananchi wa Kagera kwa kupitia Kamati ya Maafa ya mkoani humo.
“Michango yote hii tutaratibu nasi tutatumia njia yetu ya kuwashukuru kimaandishi. Kwa kupitia michango hii ndio mnaona Kagera imetulia. Kwa niaba ya wana Kagera na Serikali tunawashukuru, muendelee kujitokeza ili wenzetu waendelee na maisha yao kama kawaida. Mungu aendelee kuwaongezea pale mlipotoa,” alisema Majaliwa.
Taasisi zilizowasilisha mchango huo ni Kampuni ya simu ya Vodacom na Vodacom Foundation waliotoa Sh milioni 100, Mfuko wa Pensheni wa LAPF (Sh milioni 20), Taasisi ya kidini ya Ahmadiya (Sh milioni nne) na vifaa vya ujenzi vya thamani ya Sh milioni sita.
Nyingine ni Kampuni ya ujenzi ya Advent iliyotoa tani 40 za saruji za thamani ya Sh milioni 16.5, Taasisi ya The Art of Living Foundation iliyotoa unga wa ngano, mahindi, mchele na dawa za Sh milioni 10 pamoja na kundi la mtandao wa kijamii la WhatsApp linalojulikana kama Uongozi and Leaders Forum Groups linalohusisha viongozi mbalimbali wa serikali, viongozi wastaafu, wahadhiri wa vyuo vikuu na wanahabari ambalo limetoa Sh milioni 16.
Tetemeko hilo lilitokea Jumamosi, Septemba 10, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine 440 walijeruhiwa kati yao watu 253 walifikishwa Hospitali ya Mkoa, 153 walilazwa, 113 walitibiwa na kuruhusiwa na wengine 38 wanaendelea na matibabu ambapo kati yao watu 23 wamefanyiwa upasuaji mkubwa na wanaendelea vizuri.


Pia tetemeko hilo limesababisha nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi baada ya kupata nyufa na 9,471 zimepata uharibifu mdogo huku wananchi 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.

waziri Kindamba Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu mpya TTCL


Rais Dkt. John Magufuli, amemteua Waziri Kindamba kuwa Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL.
Taarifa ya Ikulu jijini Dar es Salaam imesema uteuzi huo ni kufuatia hatua ya Serikali kununua hisa zote za Bharti Airtel ambaye alikuwa mbia mwenza wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na hivyo Serikali kumiliki hisa za Kampuni hiyo kwa asilimia 100.
Kindamba ameteuliwa kushika nafasi hiyo kuanzia leo tarehe 23 Septemba, 2016.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kufuatia uteuzi huo, aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Dkt. Kamugisha Kazaura atapangiwa kazi nyingine.

Hospitali ya kisasa Mloganzila kuanza Januari

HOSPITALI ya kisasa ya kufundishia wataalamu wa afya na kutoa huduma ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) iliyopo eneo la kampasi ya Mloganzila jijini Dar es Salaam, inatarajiwa kufunguliwa rasmi na kuanza kutoa huduma Januari mwakani.

Hospitali hiyo iliyojengwa kisasa kwa kutumia mifumo mbalimbali ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), itakuwa ya kwanza kutumia mfumo wa teknolojia ya sampuli hewa, unaochukua vipimo kwa mtambo maalumu na kuwasilisha majibu kwa njia ya mtandao na itakuwa na wadi ya watu mashuhuri akiwemo Rais.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ziara maalumu katika jengo hilo lililokamilika ujenzi wake tangu Agosti mwaka huu, Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Profesa Ephata Kaaya, alisema hospitali hiyo, itatoa tiba ya magonjwa yakiwemo sugu kama vile moyo, saratani na figo.
Amesema hospitali hiyo, imejengwa na kufungwa vifaa tiba vya kisasa vya dijitali, vinavyotumia zaidi teknolojia ya Tehama zikiwemo mashine za X-ray, MRI, CT-Scan, mashine maalumu kwa ajili ya kupimia magonjwa ya wanawake, mashine maalumu za kupima na kutibu meno, koo, masikio na pua.
“ amesemaPia tumefunga mtambo wa kisasa zaidi wa sampuli hewa uliopo katika kila idara na kuunganishwa na maabara ambao kazi yake ni kusafirisha vipimo na kupeleka sehemu mbalimbali na majibu ya vipimo hivyo huwasilishwa sehemu husika kwa njia ya mtandao,”
Amesema mtambo huo, unasaidia kupunguza tatizo la msongamano katika chumba cha maabara, unaongeza ufanisi na usahihi wa vipimo lakini pia hupunguza muda na kuepusha mkanganyiko wa vipimo. Profesa Kaaya amesema hospitali hiyo pia itatoa huduma za kufundishia, kufanya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali na tafiti za fani za afya.
Ameeleza kuwa “Lakini pia wana vyumba maalumu 12 kwa ajili ya wagonjwa wenye magonjwa ambukizi kama vile ebola, kipindupindu na kifua kikuu,” alisema.
Amesema jengo la hospitali hiyo lina ghorofa tisa ambazo zinajumuisha vyumba 13 vya upasuaji kikiwemo chumba kimoja cha upasuaji kwa wagonjwa wa dharura, maabara za kisasa, vyumba vya wagonjwa mahtuti na kusafisha figo, wodi za kujifungulia, chumba cha kuhifadhi maiti na vyumba vya kufundishia.
Aidha amesema katika eneo la wodi zipo wodi 12 za wagonjwa mashuhuri vikiwemo vyumba viwili vyenye mitambo ya kisasa ya kufuatilia hali ya mgonjwa vya viongozi wenye hadhi ya juu akiwemo Rais.
Profesa Kaaya, amesema ujenzi wa hospitali hiyo uliogharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 94.5 katika eneo hilo la Mloganzila lenye ukubwa wa ekari 3,800, ulianza tangu mwaka 2014 kupitia mkopo wenye riba nafuu ambao malipo yake yataanza kulipwa baada ya miaka 15 kwa kipindi cha miaka 25.

Kwa mujibu wa Profesa Kaaya, hospitali hiyo itakayokuwa pia ya rufaa, itasaidia kupunguza idadi kubwa ya wagonjwa wenye magonjwa sugu kwenda nje ya nchi kutibiwa kwani itatoa tiba na vipimo vya magonjwa mengi sugu yanayosumbua Watanzania.