Tuesday, June 26, 2012

Adhabu dawa za kulevya sasa kifungo cha maisha

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi
Serikali inaandaa Muswaada wa Marekebisho ya Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya ili kuondoa adhabu ya faini na kubaki na kifungo cha maisha jela.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni miongoni mwa mikakati ya kuviwezesha vyombo vya dola kuwakamata vigogo wa biashara hiyo haramu.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alitangaza hatua hiyo jana wakati alipokuwa akizungumzia Maadhimisho ya Siku ya Dawa za Kulevya Dunia, yatakayofanyika Tandale, jijini Dar es Saalaam.

Alisema muswaada huo utawasilishwa bungeni kabla ya mwaka huu kumalizika.

Alisema sheria ya sasa ina mapungufu mengi, ikiwemo kugongana na sheria nyingine hivyo kutoa mwanya kwa biashara hiyo kushamiri.

Aliyataja mapungufu hayo ni sheria hiyo kutoa mwanya kwa hakimu kumhukumu mtu aliyepatikana na kosa kulipa faini kwa dawa za kulevya ambazo hazizidi thamani ya Sh. milioni 10.

“Hivi mmeshawahi kusikia mtu amehukumiwa miaka 30 ingawa sheria inaanisha hukumu hiyo?” alihoji na kuongeza:  “Ni mmoja tu aliwahi kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.”

Alisema sheria hiyo imetoa mwanya kwa vigogo wa biashara hiyo kukwepa mkono wa sheria kwa sababu vijana wanapokamatwa na dawa hizo huogopa kuwataja kwa kuhofia kukosa mtu wa kuwalipia faini.

“Hii sasa itawawezesha kuacha woga kuwataja kwa sababu hawatahofia usalama wao kwa kuwa watahukumiwa maisha yao yote jela,” alisema.

Lukuvi alisema pia suala la kupeleka vidhibiti vya dawa za kulevya mahakamani wakati wote wa uendeshaji wa kesi limekuwa kikwazo kikubwa kwa kuwa dawa hizo zimekuwa zikipungua ubora kwa kadri muda unavyoendelea.

Pia alisema kutunzwa kwa dawa hayo kama ushahidi kumekuwa kukisababisha vishawishi vya kuziiba.

Alisema katika mabadiliko hayo watapendekeza cheti cha Mkemia Mkuu wa Serikali kinachothibitisha kuwa ni dawa za kulevya kitumike kama ushahidi mahakamani badala ya kupeleka ushahidi wa dawa hizo hadi hukumu itakapotolewa.

Kadhalika, alitolea mfano wa mapungufu ya sheria hiyo kuwa hata mtambo ambao ulikamatwa Mbezi, jijini Dar es Salaam wa kutengeneza dawa za kulevya mahakama iliwaamuru kurejesha kwa wamiliki.

Pia magari ambayo yamekamatwa yakiwa na dawa za kulevya katika maeneo mbalimbali nchini, mahakama imeamuru kurejeshwa kwa wamiliki.

Akizungumzia kuhusiana na harakati za kupambana na dawa hizo, Lukuvi, alisema katika kipindi cha Januari hadi Mei, 2012 kiasi cha kilo 234 za Heroin kimekamatwa, ambacho ni kikubwa sana katika kipindi kifupi.

“Maadhimisho haya yamekuja katika kipindi ambacho kumekuwa na ongezeko kubwa la usafirishaji wa kiasi kikubwa cha dawa za kulevya nchini hasa viwandani, zikiwemo Heroin na Cocaine,” alisema.

Alisema ongezeko hilo linaashiria kuwepo kwa ongezeko la matumizi ya dawa hizo nchini.

Akitoa takwimu za watu waliokamatwa na dawa za kulevya nchini, Lukuvi alisema mwaka 2007 wanaume 7646 na wanawake 806 walikamatwa na dawa za kulevya wakati mwaka 2008 wanaume 6,230 wanawake ni 367.

Mwaka 2009 wanaume 3,751, wanawake 263, mwaka 2010 wanaume walikuwa ni 51 wanawake 11, mwaka juzi wanaume 93, wanawake 11, wakati mwaka huu wanaume ni18 na wanawake wanne.

Alisema hadi kufikia Januari hadi Mei mwaka huu, jumla ya kilo 234.061 za Heroin na Cocaine kilo 16.845 zilikamatwa.

Lukuvi pia alisema jumla ya waathirika 15,942 walihudhuria vituo vya tiba kuanzia mwaka 2008 hadi 2010.

 Vile vile, alisema Watanzania 211 walikamatwa wakijihusisha na biashara hiyo nje ya nchi katika kipindi cha mwaka 2005 hadi 2010 na miongoni mwao walihukumiwa kunyongwa, huku wengine wakitumikia adhabu za vifungo.

Alisema kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni ‘Tujenge Jamii yenye afya bila dawa za kulevya: Tutoe maoni ya Katiba na kushiriki sensa ya Mwaka 2012’.

Alisema mgeni rasmi katika maadhimisho hayo yatakayofikia kilele chake Juni 26 mwaka huu, atakuwa ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Alisema kilele cha maadhimisho hayo kitatanguliwa na maandamano ambayo yataanzia Manzese Darajani wilayani Kinondoni na kuishia kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Tandale.

No comments:

Post a Comment