UAMUZI
wa Serikali kuondoa kodi ya mapato kwa wafanyabiashara wa kusafirisha
abiria kupitia pikipiki maarufu kama bodaboda, umepokelewa kwa hisia
tofauti na wananchi hasa baada ya kutolewa hoja wengi, wanaonufaika na
biashara hiyo sio vijana wanaoendesha bali ni wamiliki ambao wengi wao
ni maofisa , wafanyabiashara wakubwa na watumishi wa sekta nyingine.
Naibu
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Hezron
Kaaya alisema Serikali inapaswa kutumia vyombo vyake ili kufanya
uchunguzi ni kina nani wamiliki wa bodaboda badala ya kufikia uamuzi ya
jumla kuondoa kodi.
Alisema kama Serikali ina nia ya dhati
kuwasaidia, waendesha bodaboda ilazimishe wawe na mikataba na waajiri na
wawalipe vizuri tofauti na sasa ambapo wanatakiwa kuwafikishia wamiliki
wa bodaboda kati ya Sh 15,000 na 20,000 kwa siku na wao wakijitafutia
kipato nje ya fedha hizo.
“Sisi hatupingi kufutwa kodi ila
tunataka Serikali itazame biashara hii kwa ujumla wake ili kweli
iwasaidie vijana”alisema Kaaya.
Alisema Serikali inachopaswa
kufanya ni kuongeza wigo wa kupata watu wengi wanaolipa kodi kwani sasa
wafanyakazi wa umma ndio wanapata shida kwa kulipa kodi ya mishahara ya
Payee kubwa na wao ndio sasa walipa kodi wakubwa.
Naye Ismail
Kayanda alifafanua kuwa, hoja ya kuondolewa kodi hiyo, inakuwa na
manufaa kwani vijana wengi wamejiajiri katika kazi ya bodaboda na kuwa
na vipato vya uhakika.
Kayanda alisema tangu biashara ya
bodaboda ianze makundi ya vijana, wasio na ajira ambao walikuwa kero
hasa nyakati za usiku, imepungua.
“Hapa Dodoma ulifika wakati
ukitembea usiku unakuwa na hofu ya kukumbwa na vijana lakini sasa
vijana hao hao, tunawaona wametulia wanafanyakazi ya bodaboda,”alisema
Kayanda.
Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, akihitimisha hotuba
ya bajeti, alieleza kukubaliana na hoja ya wabunge, ikiwamo kamati ya
Uchumi na Fedha ambayo ilishauri kuondolewa kwa kodi hiyo na pia kodi
kwa wafanyabiashara wadogo au vipato vyao havijafikia 3 milioni. |
No comments:
Post a Comment