Thursday, June 7, 2012

Chadema wamkataa Chenge

John Mnyika
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, hana mamlaka ya kimaadili kuingoza Kamatiya Bunge ya Fedha na Uchumi.

“Chadema tumeshangazwa kwa kuchaguliwa kwa aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge, kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi,” alisema Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika.



Mnyika aliyekuwa anazungumza kwenye mikutano ya hadhara katika vijiji mbalimbali vya Kata za Lumesule na Napacho, wilayani Nanyumbu juzi na alisema kwa vile Chenge ni miongoni mwa watu wanaotajwa katika tuhuma nzito za ufisadi, anakosa mamlaka ya kimaadili kushika wadhifa nyeti kwa taifa kama huo.


Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, alidai kuwa kuchaguliwa kwa Chenge kuiongoza kamati hiyo kuna athari kubwa kwa taifa kutokana na kuongeza idadi ya watuhumiwa wa ufisadi wanaozingoza Kamati za Bunge.


“Walianza kukiteka chama chao cha CCM, ambacho kimeshindwa kuwachukulia hatua, badala yake kinapiga kelele za kupinga ufisadi barabarani, huku watuhumiwa wakiendelea kutamba kwa kushika nafasi mbalimbali serikalini na bungeni, sasa wanaingia bungeni,” alisema.


“Jamani Watanzania wenzangu, wananchi wa Lumesule mnajua kuwa CCM kimeshatekwa na mafisadi, kwanza tulipotangaza orodha ya mafisadi na ufisadi wao pale Mwembeyanga walikataa kuwa ndani ya chama chao hakuna mafisadi. Baadaye wakakiri wao wenyewe wakisema wanajivua magamba, yaani watuhumiwa wa ufisadi waondoke ama watawafukuza,” alisema.


“Chenge yule mnayemfahamu kama mmoja wa watuhumiwa wa ufisadi nchini, amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Uchumi, moja ya kamati nyeti kabisa katika bunge letu,” alisema na kuongeza:


“Sasa hii ni hatari, watuhumiwa wa ufisadi walianza kuiteka serikali ya CCM kwanza, kisha wakakiteka kabisa chama chao.”


Mnyika alisema Kamati ya Fedha na Uchumi ni nyeti inayoisimamia serikali katika masuala muhimu ya uchumi, ikiwemo maandalizi ya bajeti ya nchi kabla haijafikishwa mbele ya Bunge zima, hivyo kuchaguliwa kwake kunatoa tafsiri ya kukabidhiwa mikoba ya kusimamia fedha za Watanzania kupitia kamati hiyo.


Alisema Chenge ataongoza jukumu la kusimamia ‘chenji’ zinazotokana na kashfa ya ununuzi wa rada, ambayo yeye pia ni mtuhumiwa.


NIPASHE jana lilimtafuta Chenge kuzungumzia tuhuma hizo hakutapikana kutokana na simu yake ya kiganjani kuzimwa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi, hakujibu hadi tunakwenda mitamboni.


MBOWE ‘KUWAVAA’ MEMBE, GHASIA


Wakati Mnyika akielekeza ‘mashambulizi’ ya chama hicho kwa Chenge, Kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe, amejitwisha ‘zigo’ la kumbana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, kutokana na viongozi wa serikali za mitaa, vijiji na madiwani, kutoitisha mikutano ili kuwasomea wananchi hesabu za mapato na matumizi ya fedha za umma.


Alisema usomaji wa hesabu hizo unaopaswa kufanyika kila baada ya miezi mitatu ni kwa mujibu wa sheria za nchi.


Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema na Mbunge wa Hai, alitoa kauli hiyo juzi katika mkutano wa hadhara wa Operesheni Okoa Kusini uliofanyika Makanga wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara.


Alisema pamoja na kuibana serikali kuhusu sakata la serikali kuwakopa korosho wakulima wa Mtwara, atahakikisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Ghasia wanatoa jawabu la kero zilizotolewa na wananchi wa maeneo tofauti mkoani humo.


Mbowe alisema kero zilizowasilishwa kwake na wakazi wa Nanyumbu wilayani Masasi kuhusu kero wanazozipata wanapoingia Msumbiji ni matokeo ya sera mbovu za uhusiano wa kimataifa ambazo zinawafanya Watanzania kunyanyaswa tofauti na wageni wanapoingia nchini.


Azma ya Mbowe ilitokana na kauli ya mkazi wa kata ya Makanga, Mkapura Omary, aliyedai kuwa kumekuwepo unyanyasaji unaofanywa na maofisa wa Uhamiaji kwa Watanzania wanaoingia nchini humo, licha ya kufuata sheria na taratibu zilizopo.


“Tunakuomba utusaidie kwa maana tunaonewa kila tunapovuka kwenda Msumbiji kupitia daraja la Umoja,” alidai na kutoa mfano kuwa aliwahi kunyang’anywa mali zake akiwa nchini Msumbiji, lakini hakupata msaada ambao ungemwwezesha kuzirejesha.


Omary alidai kuwa ingawa alifanikiwa kurejea nchini baada ya sakata hilo, wenzake watatu aliokuwa nao na ambao hakuwataja kwa majina, wamekwama nchini humo wakiendelea kutaabika.


Hata hivyo, akijibu hoja hiyo, Mbowe alisema vitendo hivyo na vingine vya aina hiyo ni matokeo ya nchi kuwa na sera mbovu zinazohusiana na masuala ya ushirikiano wa kimataifa, kiasi cha kuwakumbatia wageni na kushindwa kuzishughulikia kero za raia wanapokuwa nje ya nchi.


“Nitakwenda bungeni na kumhoji Membe kuhusu suala hilo ili kuona namna sisi kama taifa tunavyopaswa kuchukua hatua,” alisema.


Akizungumzia suala la viongozi wa vijiji, mitaa na madiwani kushindwa kusoma taarifa za mapato na matumizi ya fedha za umma, Mbowe alisema atalielekeza suala hilo kwa Ghasia.


“Nitataka Waziri wa Tamisemi atueleze ni hatua gani anachukua dhidi ya viongozi hao, ama nini anajua kuhusiana na viongozi kutofanya mikutano na kuwasomea wananchi mapato na matumizi ya vijiji na kata zao wakati ni haki ya msingi kwa mujibu wa sheria,” alisema.

 AMGOMEA OCD

Katika hatua nyingine, Mbowe alijikuta akipinga hoja ya ofisa wa polisi aliyesemekana kuwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nanyumbu, alipomtaka ashuke jukwaani kwa madai kuwa muda wa kuhutubia ulikuwa umepiga.


Ofisa huyo alimtuma mmoja wa viongozi wa Chadema amfikishie ujumbe Mbowe, kwamba alitakiwa kukatisha hotuba yake na kushuka jukwaani, ndipo Mbowe aliposema na kuhoji:


“Mimi ni Mbunge na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, OCD sikiliza usitutishe, tumetembea maelfu ya kilomita kwa ajili ya kuwaokoa Watanzania wakiwemo watoto wako…unakuja kuniambia funga mkutano?”

Kwa mujibu wa Mbowe, muda wa kuhutubia mkutano huo ulikuwa bado unampa fursa ya kuzungumza na wananchi wa Nanyumba, jimbo lililowahi kuwakilishwa na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.

Hivyo, aliendelea kuhutubia na mwishowe kuuza kadi na kuorodhesha majina ya wanachama wapya, wakiwemo waliojitokeza kuyaongoza matawi ya Chadema kwa muda, kabla ya kufanyika uchaguzi baadaye mwaka huu.


Chadema ilimaliza mikutano yake ya Operesheni Okoa Kusini iliyofanyika mkoani Mtwara jana na leo wanaanza mikutano kama hiyo kwenye vijiji, kata na wilaya za mkoa wa Lindi.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment