Na Daniel Mjema,Moshi MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi mkoani Kilimanjaro,imemhukumu kifungo cha miaka miwili
jela, dereva wa lori moja la mafuta baada ya kupatikana na hatia ya
kuchakachua mafuta aina ya disel.
Awali upande wa mashitaka
ukiongozwa na wakili wa serikali kanda ya Moshi, Jullius Semali ulidai
kuwa mshitakiwa huyo, Winter Aloyce Mushi alitenda kosa hilo Agosti 17
mwaka 2011.
Ilidaiwa siku hiyo,akiwa na lori hilo likiwa na lita
37,000 mali ya kampuni ya Panone & Company Ltd, mshitakiwa
alichakachua lita 6,000 za mafuta aina ya Diesel yenye thamani ya
sh12,630,000.
Akisoma hukumu hiyo jana mjini Moshi, Hakimu Mkazi
Munga Sabuni alisema mahakama hiyo imeridhika bila shaka yeyote na
ushahidi uliotolewa na mashahidi watano wa upande wa mashitaka.
Sabuni
alifafanua kuwa ushahidi wa mashahidi hao akiwamo mmoja kutoka Mamlaka
ya Udhibiti wa huduma ya Nishati na Maji (Ewura), ulithibitisha mafuta
hayo yalikuwa yamechakachuliwa.
“uchunguzi wa kimaabara
ulionyesha kiwango cha density (ubora) kilikuwa kimeshuka kutoka 831
hadi 827 na hakuna mtu mwingine aliyekuwa amekabidhiwa mafuta hayo zaidi
ya mshitakiwa”alisema.
Hakimu huyo alisema kuwa kwa kuwa vitendo
vya uchakachuaji mafuta vimekuwa na athari kimazingira na vyombo vya
moto,mahakama inamhukumu kifungo cha miaka miwili jela ili iwe fundisho
kwa wengine. |
|
No comments:
Post a Comment