Wednesday, June 27, 2012

Mkakati wa kumsaka Kony kujadiliwa leo

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa leo kujadili mkakati wake wa kumsaka kiongozi wa kundi la waasi la Lord's Resistance Army, LRA, Joseph Kony.
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Afrika, Francisco Madeira, amewaambia waandishi wa habari mjini New York, Marekani hapo jana kwamba kikosi maalumu cha wanajeshi huenda kikaanza kufanya kazi mwezi Desemba mwaka huu, iwapo kitapata vifaa vinavyohitajika.

 Kufikia sasa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Sudan Kusini na Uganda, zimekubaliana kutoa wanajeshi 5,000 kuliangamiza kabisa kundi la Kony.
 Mwaka jana rais wa Marekani, Barack Obama, alituma washauri 100 wa kijeshi kusaidia kumtafuta Kony. Kiongozi huyo wa waasi anatafutwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC, mjini The Hague, Uholanzi, kwa uhalifu wa kivita na uhalifi dhidi ya ubinaadamu.
 Anashutumiwa kwa kuwateka nyara watoto na kuwatumia kama wanajeshi na watumwa wa ngono.

No comments:

Post a Comment