MWANDISHI
WA BBC AMSHUHUDIA AKIPUMULIA MASHINE KATIKA HOSPITALI MOJA AFRIKA
KUSINI, MKUU WA JOPO LA MADAKTARI ALIYEMTIBU DAR AONGEAWaandishi Wetu, Dar na Afrika Kusini AFYA
ya Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka
aliyeanza matibabu akiwa chini ya uangalizi maalumu wa madaktari (ICU),
baada ya kutekwa, kupigwa na kisha kutupwa kwenye pori la Pande nje
kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, ni mbaya, Mwananchi limeelezwa.Habari
zilizolifikia gazeti hili jana zilieleza kuwa daktari huyo wa magonjwa
ya binadamu, sasa hajitambui na anapumulia mashine katika moja ya
hospitali za nchini Afrika Kusini alikolazwa kwa matibabu hayo.
Dk
Ulimboka ambaye awali kulizuka utata wa mahali alipo; Afrika Kusini au
Ujerumani, sasa imethibitika kuwa yuko Afrika Kusini, lakini hali yake
ni mbaya.
"Ukweli ni kwamba yuko Afrika Kusini, lakini taarifa
tulizozipata leo (jana) asubuhi ni kwamba sasa amelazwa ICU akiwa
hajitambui kabisa," alisema mmoja wa madaktari wanaofuatilia kwa karibu
matibabu ya Ulimboka.
Aliendelea, "Sasa hajitambui na tumwombe Mungu tu afanye miujiza yake."
Kiongozi
wa Jopo la Madaktari linaloshughulikia matibabu ya Dk Ulinboka, Profesa
Joseph Kahama alisema amezisikia taarifa hizo zikitangazwa na Kituo cha
Utangazaji cha Uingereza, (BBC) jana asubuhi, lakini hajaweza
kuzithibitisha.
"Asubuhi wote tulisikia kwamba hali yake (Dk
Ulimboka) ni mbaya na yuko kwenye 'koma', lakini taarifa hizo
sijazithibitisha kujua zina ukweli kiasi gani," alisema. Mwananchi
liliwasiliana na mwandishi wa BBC Afrika Kusini, Omary Mutasa ambaye
alisema kwamba, ni kweli alikwenda kwenye hospitali (jina linahifadhiwa
kwa sasa) alikolazwa Dk Ulimboka ambako alimkuta akipumua kwa usaidizi
wa mashine na alikuwa hawezi kuongea.
“Niliingia hadi sehemu
alikolazwa Dk Ulimboka, nimeona akipumua kwa usaidizi wa mashine, hata
ndugu zake walishtuka sana kuniona pale na hawakufurahishwa mimi kwenda
pale,” alisema katika mahojiano ya simu na Mwananchi.
Mutasa alisema kwamba, jana jioni alikwenda hospitali kuangalia hali yake inaendeleaje, lakini hakuweza kumwona.
“Nimejaribu
kwenda tena jioni kupata taarifa za hali yake, lakini nimeshindwa
kumwona. Utawala wa hospitali ulinikatalia kabisa,” alisema.
Jana
asubuhi, Mutasa aliripoti katika kipindi cha asubuhi cha BBC kwamba
hali ya Dk Ulimboka ni mbaya na kalazwa katika chumba cha wagonjwa
mahututi na anapumulia mashine.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama
Cha Madaktari (MAT), Dk Rodrick Kabangila alisema haelewi uvumi huo
umetoka wapi kwani yeye hana taarifa hizo.
“Mimi bado nashindwa
kuelewa kwani nimezungumza na na wenzangu ambao wanawasiliana na ndugu
wa Dk Ulimboka kwa karibu wakasema hakuna taarifa zozote zile mbaya,”
alisema Dk Kabangila. Naye Rais wa Chama hicho, Dk Namala Mkopi alisema hajawasiliana na Dk Ulimboka tangu juzi. “Bado sijawasiliana na Dk Ulimboka na hatujapata taarifa zozote za hali yake kama ni mbaya au vipi,” alisema Dk Mkopi.
Mbowe ataka uchunguzi Katika
hatua nyingine, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe,
ameitaka Serikali kuifanyia kazi Sheria ya Uchunguzi wa vifo vyenye
utata kama ilivyoahidiwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika kikao cha
bajeti mwaka jana.
Akizungumza katika kipindi cha Maswali na
Majibu kwa Waziri Mkuu, Mbowe alisema kutotimizwa kwa ahadi hiyo
kunaleta hisia kwamba Serikali inahusika katika baadhi ya vifo hivyo.
Mbowe
alisema kuwapo kwa vifo vya aina hiyo nchini huku baadhi yake
vikihusishwa na vyombo vya dola, kunahitaji uchunguzi wa kina na
yakinifu utakaofanywa na chombo huru ili kubaini wahusika na kisha
kuwachukulia hatua za kisheria.
“Katika hotuba yako Waziri Mkuu
ulikiri kuwepo kwa tatizo hilo na ulisema sheria ya uchunguzi wa vifo
vyenye utata itafanyiwa kazi na vifo vyenye utata vitafanyiwa uchunguzi,
pengine unaweza kutwambia ni upi utekelezaji wa ahadi yao hiyo?”
alisema Mbowe wakati anamwuliza swali Waziri Mkuu.
Mbowe alisema
hisia za dola kuhusika katika mauaji na mateso haya ya raia zimekuwa
zikikuwa kila kukicha na hivyo taifa limepata sifa mbaya katika anga za
kimataifa hasa baada ya kipigo cha Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, Dk
Stephen Ulimboka na wabunge wa Chadema jijini Mwanza. Akijibu swali hilo Waziri Pinda alisema si kweli kuwa taifa linapata sifa mbaya kutokana na tukio la kupigwa kwa Dk Ulimboka.
“Sikubaliani
na hoja kuwa sifa ya nchi imeharibika. Kwa lipi? Ukisema hivyo uwe na
ushahidi wa hilo. Vilevile ukitumia mfano wa Ulimboka si mzuri. Jambo
hili linahitaji kupatikana ukweli kwanza. Sasa tumeagiza uchunguzi wa
kina na wa haraka kufanyike ili tupate ukweli huo,” alisema Pinda.
Kuhusu
sheria ya uchunguzi wa vifo vyenye utata, Waziri Mkuu Pinda alisema ni
kweli aliahidi kwamba sheria inahitaji kufanyiwa marekebisho na kwamba
tayari vyombo husika vimepewa maelezo ili kuwezesha mabadiliko hayo
kufanyika.
“Wakati mwingine ni uzembe na ufuatiliaji duni. Si
kweli kuwa Serikali inahusika. Sisi (Serikali) tutaendelea kufuatilia
jambo hilo kwa umakini na kuhakikisha sheria hiyo inaanza kufanya kazi,”
alisema Pinda.HABARI KWA HISANI YA GAZETI LA MWANANCHI |
No comments:
Post a Comment