Thursday, January 9, 2014

Waziri Nagu awataka wadau wa sukari kuwa wazalendo


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya sukari Tanzania, Bw. Henry Semwaza (kushoto) wakati wa mkutano wa siku moja wa wadau wa sukari nchini uliofanyika jana Mkoani Morogoro. Wengine ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza (wa pili kulia) na Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha sukari cha TPC Moshi, Bw. Robert Baissac.
Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji Dkt. Mary Nagu (kushoto) akibadilishana mawazo na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza (katikati) muda mfupi mara baada ya kufungua mkutano wa wadau wa sukari uliofanyika jana mkoani Morogoro. Kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha sukari cha TPC Moshi, Bw. Robert Baissac.

Na Mwandishi wetu, Morogoro

Serikali imewataka wadau wa sukari nchini, kuwa na uzalendo wa hali ya juu katika uzalishaji na uuzaji wa bidhaa hiyo muhimu, kwani kwa kufanya hivyo watapunguza matatizo yanayojitokeza mara kwa mara na malalamiko miongoni mwa wananchi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu aliyasema hayo mkoani Morogoro jana wakati akifungua mkutano wa siku moja wa wadau wa sukari.

“Ni matumaini yangu kuwa wadau wote kwa pamoja tuwe wawazi, wakweli na waaminifu kwa wale wote wanaotutegemea,”alisema waziri Nagu.

Aliongeza kuwa sekta ya kilimo inahitaji utulivu wa hali ya juu sana, na kuwa kwa kuwepo utulivu huo kutasaidia kuleta manufaa kwa ngazi zote, kuanzia mzalishaji mdogo, wa kati mkubwa na mlaji.

“Wakulima wasipofanya vizuri kwa sababu wana malalamiko yao viwanda vitaathirika, na hivyo kutoa nafasi kwa wafanyabiashara ambao wanaweza kukimbilia nje ya nchi kutafuta bidhaa hiyo,” aliongeza Dkt. Nagu.

Akizungumzia kuhusu uhuru wa soko, Dkt. Nagu alisema pakiwa na mwenendo mzuri wa soko huru, mambo yote yataenda vizuri, lakini kama soko haliendi vizuri na hakuna wakulisimamia ni lazima pawepo na matatizo.

“Jukumu letu la leo ni kuona kwamba soko hili huru linafaidisha kila mtu,” alisisitiza.
Amesema ili kuondoa malalamiko ya mara kwa mara kwa wananchi hasa katika zao hili la sukari ni lazima viongozi wawe mstari wa mbele kulisimamia hasa wanapoona sukari inakua juu pasipo sababu ya msingi.

“Katika usimamiaji wa bidhaa hii ya sukari inabidi tuchukue hatua ambazo zitafanya eneo hili kuwa endelevu na sio hatua za muda mfupi ambazo hazimalizi matatizo yaliyopo ,” aliongeza.

Alisema viwanda vya sukari vinatakiwa kufanyakazi kwa ufanisi unaotakiwa na kuwa hiyo  itafanyika endapo viwanda hivyo vitakubali changamoto zilizopo katika uzalishaji wa bidhaa hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma Kutoka kituo cha uwekezaji Nchini (TIC) Bi. Nakuala Senzia alisema kuwa mkutano huo umekuwa muhimu hasa kwa kuwakutanisha wadau hao na kusema kuwa eneo la uwekezaji katika eneo hilo ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi.

“Sisi kama TIC tupo hapa kuangalia fursa mbalimbali za uwekezaji, hivyo ni jukumu letu kutoa maelekezo na kuwaeleza wawekezaji kuwa bado maeneo ni mengi ya kuwekeza katika nchi hii hasa kwa zao la sukari,” alisema.

Aliongeza kuwa zao la sukari ni muhimu sana kwa matumizi ya watu hivyo ni vyema uzalishaji ukawa wa kutosha ili kuepusha malalamiko kwa wananchi.

“Hivi sasa tuna maeneo mengi ambayo tutayalenga kwa ajili ya uwekezaji hasa katika zao la miwa ili kuweza kuongeza uzalishaji wa sukari,”alisema.

Aliyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni Ngalimila wilani kilombero, Mkulazi katika wilaya ya Morogoro pamoja na Bagamoyo.
Alisema maeneo hayo yote tayari yapo na kinachofanyika sasa ni upembuzi yakinifu wa maeneo yote, ili kubaini ni zao gani liwepo katika eneo husika.


Mkutano huo wa siku moja uliwakutanisha wadau wa sukari kutoka katika viwanda vya Mtibwa, Mkoani Morogoro, Kagera sukari kutoka Kagera, TPC Kilimanjaro, kiwanda cha kilombero pamoja na wadau kutoka serikalini.

No comments:

Post a Comment