Mtandao wa kupinga ukeketaji Tanzania unaoshirikisha mashirika 12 ambayo ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), WOWAP, DIAC, NAFGEM, TAWLA,TAMWA, AFNET,CCT, CDF, BAKWATA, HOUSE OF PEACE, na WORLD VISION, utafanya maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ukeketaji Duniani.
Maadhimisho hayo yalifanyika katika kijiji cha Ngimu Mkoani Singida mnamo Tarehe 6/2/2014, kwa uratibu wa mmoja wa wanachama wa Mtandao Jumuhiya ya Kikristo Tanzania (CCT). Singida ni moja ya mikoa ambayo ukeketaji unafanyika kwa kiwango kikubwa na CCT wanafanya kazi kubwa mkoani humo katika kuhamasisha jamii kuachana na tabia hii.
Maadhimisho ya mwaka huu yanalenga kujenga nguvu mpya ili kuakikisha kuwa kiwango cha Ukeketaji kinashuka kutoka asilimia 15 ya sasa hadi sifuri.Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Ukeketaji haukubaliki- ACHA!!”
Kama mnavyofahamu kampeni hii ni ya kimataifa na sehemu zoteulimwenguni ambapo vitendo hivi vinafanyika kuna maadhimisho haya ya kila mwaka kupinga ukeketaji. Hapa Afrika ni nchi 28 ndizo vinara wa ukeketaji ikiwamo Tanzania
Takwimu za Taarifa ya Demographia ya mwaka 2012 zinaonyesha kuwa Ukeketaji uko kwa kiwango kikubwa katika mikoa iliyo mingi hapa Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mikoa inayoongoza kwa ukeketaji na takwimu zake ni kama ifuatavyo: Manyara (71%), Arusha (55%), Mara (40%). Vilevile taarifa zinazoonyesha kwamba katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo kwa ukeketaji unaofanywa kwa watoto wachanga hasa katika wilaya za Manyoni Mkoani Singida.
Takwimu hizi kwa ujumla zinatisha kwani ikumbukwe kuwa Ukeketaji una madhara makubwa kwa afya ya mtoto wa kike na mwanamke ikiwamo matatizo ya fistula, kushindwa kuzuia haja ndogo na kubwa, kupata shida sana wakati wa kujifungua ikiwemo; kuchanika vibaya wakati wa uzazi na kupata maumivu wakati wa kufanya tendo la ndoa, ikiwemo athari za kisaikolojia.
Kampeni yetu mwaka huu imemualika Naibu waziri wa sheria na katiba Mh; Angela Kairuki kuwa mgeni rasmi huko Singida kutokana na uzito wa swala hili.
Ni kutokana na mambo yaliyoainishwa hapo juu ndio maana sisi wanamtandao wa kupinga ukeketaji tunatoa wito ufuatao:
1. Serikali ionyeshe utashi wa kisiasa kwa kutekeleza sera na mpango wa kupinga na kutokomeza ukeketaji kwa kufuatilia utendaji wake ili kutokomeza mila kandamizi. Vilevile serikali itenge rasilimali kwa ajili ya mpango huu.
2. Sheria dhidi ya mila hii ya ukeketaji zitekelezwe na zile zinazohitaji mapitio au marekebisho zipitiwe upya.
3. Asasi za kiraia ziendelee na kampeni za ushawishi na inapobidi kupitia tena mikakati ili kuleta matokeo mazuri na ya kudumu.
4. Wadau wote wafanye kazi kwa pamoja na kushirikiana ili kuleta matokeo chanya. Mtandao wa kupinga ukeketaji unahitaji kuimarishwa.
5. Rasilimali watu na fedha zitengwe ili kusaidia kutokomeza mila hii kwa kutumia nyenzo zilizopo sasa ikiwemo utekelezwaji wa sheria ya kanuni ya adhabu.
“Ukeketaji haukubaliki, hauvumiliki- ACHA!”
Tamko hili limetolewa kwenu na mashirika yafuatayo;
1. LHRC- Legal and Human Rights Centre
2. WOWAP- Women Wake Up, Dodoma
3.DIAC- Dodoma Inter - Africans Committee
4. NAFGEM -Network Against Female Genital Mutilation
5. TAWLA - Tanzania Women Lawyers Association
6. TAMWA - Tanzania Media Women Association
7. AFNET - Ant- Female Genital Mutilaion
8. CCT - Christian Council of Tanzania
9. CDF - Child Dignity Forum
10. BAKWATA - Muslim Council
11.HOUSE OF PEACE
12. WORLD VISION
Na kusainiwa kwa niaba yao na mkurugenzi mtendaji
Kituo cha sheria na haki za binadamu.
DR HELEN KIJO BISIMBA
No comments:
Post a Comment