Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam kwa
kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama tumejipanga ipasavyo
kuhakikisha mchezo kati ya REAL MADRID ya nchini Hispania na TANZANIA 11 ya
Tanzania wenye mvuto mkubwa kwa mashabiki wa Tanzania, nchi za Afrika
Mashariki, Afrika na duniani kote utachezwa katika hali ya usalama.
Mechi hiyo inawahusisha
wachezaji wa Klabu ya Real Madrid ambao wanafahamika katika nchi zao na kote
duniani kwa vile wameshiriki michezo ya
kimataifa ya mpira wa miguu ambao wamepata umaarufu mkubwa. Kwa kufahamu hilo
maandalizi mbalimbali ya kiusalama yamekwishafanyika ili kuhakikisha wachezaji
hao na maafisa walioambatana nao wanakuwa salama kuanzia siku ya kwanza hadi
watakapoondoka. Pia umeandaliwa utaratibu wa kuhakikisha usalama katika uwanja
wa taifa kabla, wakati na baada ya mechi hiyo.
Kutakuwa na idadi kubwa ya
askari polisi walioandaliwa mahususi kwa ajili ya mechi hiyo ya kirafiki ya
kimataifa wakishirikiana na vyombo vingine vya dola vilivyopewa majukumu maalum
ya kulinda usalama katika uwanja huo. Kila atakayeingia uwanjani atathibitishwa
kwamba ni mtu sahihi asiye na silaha au chochote chenye kuleta madhara.
Katika uwanja huo hakuna
mtu atakayeruhusiwa kukaa katikati ya ngazi za kupandia au kushukia ikiwa ni
hatua ya kudhibiti usalama. Ni marufuku kuingia uwanjani na chupa ya maji au
kimiminika chochote na endapo mtu atahitaji huduma hiyo, kutakuwa na utaratibu
maalum ulioandaliwa.
Safari hii tunategemea
walinzi maalum wa mpira (STEWART) kuongeza nguvu ya ulinzi wa kawaida na
watakuwa wanaangalia upande wa watazamaji (Jukwaani). Hivyo mtu yeyote
atakayekiuka taratibu au kusababisha hofu katika uwanja huo ataonekana na
atachukuliwa hatua kali za kisheria bila kujali nafasi yake katika jamii.
Aidha, flash- flash au aina yeyote ya milipuko iwe na sauti au la hairuhusiwa
kutumika uwanjani hapo siku ya mchezo huo muhimu.
Aidha, mafanikio katika
mechi hiyo hayataishia katika mambo ya kiusalama pekee bali pia kiuchumi hasa
katika sekta ya utalii.
S. H. KOVA
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM
No comments:
Post a Comment