Friday, October 7, 2016

Benki ya TIB Corporate yatumia wiki ya huduma kwa wateja kuboresha mahusiano na wateja wake


 Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa  TIB Corporate Bank , Bw Frank Nyabundege (Kushoto) akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mkuu wa Bohari Kuu ya Dawa nchini, Bw Laurean Bwanakunu ambae taasisi yake ni mteja wa benki hiyo wakati wa hafla fupi ya  kuadhimisha wiki ya Huduma kwa wateja Duniani iliyoandaliwa na benki hiyo jijini Dae es Salaam jana ili kutoa fursa kwa wateja wake kutoa mrejesho kuhusiana na huduma zinazotolewa na benki hiyo.
 Wafanyakazi wa  TIB Corporate Bank , wakimpokea mmoja wa wateja wakubwa wa benki hiyo,Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya PMM Estate (2001),  Dr Judith Mhina (kulia) alipohuduhuria  hafla fupi ya  kuadhimisha wiki ya Huduma kwa wateja Duniani iliyoandaliwa na benki hiyo jijini Dar es Salaam jana ili kutoa fursa kwa wateja wake kutoa mrejesho kuhusiana na huduma zinazotolewa na benki hiyo.
 Meneja Uhusiano wa Benki ya TIB Corporate, Margareth Mulenga (kushoto) na Ofisa wa benki hiyo  Jane Magingi  (katikati)  wakisalimiana na mmoja wa wateja wakubwa wa benki hiyo,Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya PMM Estate (2001),  Dr Judith Mhina (kulia) alipohuduhuria  hafla fupi ya  kuadhimisha wiki ya Huduma kwa wateja Duniani iliyoandaliwa na benki hiyo jijini Dar es Salaam jana ili kutoa fursa kwa wateja wake kutoa mrejesho kuhusiana na huduma zinazotolewa na benki hiyo
 
Katika kuadhimisha wiki ya Huduma kwa wateja Duniani,TIB Corporate Bank imekutana na wateja wake ili kujadili nafasi na mchango wa benki hiyo katika biashara huku ikitoa nafasi kwa wateja na wadau wa benki hiyo kutoa ushauri kuhusiana na huduma zake.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati hafla fupi iliyoambatana na mazungumzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Bw Frank Nyabundege alisema maadhimisho hayo ambayo ni ya kwanza kufanywa na benki hiyo tangu ianzishwe mwaka 2015 yametoa fursa kwa wateja wa benki hiyo kutoa mrejesho kuhusiana na huduma zinazotolewa na benki hiyo.

“Maadhimisho haya ya wiki moja yalianza Octoba 3 mwaka huu na tunatarajia kuhitimisha Oktoba 7, kweli yamekuwa na manufaa makubwa sana kwetu kwa kuwa tumeweza kukutana na wateja pamoja na wadau wetu mbalimbali ambao wametumia fursa hii kutupatia mrejesho kuhusiana na huduma tunazotoa,’’ alibainisha.

Bw Nyabundege aliongeza kwamba kwasasa benki hiyo imeboresha zaidi huduma zake ikiwemo suala la mikopo mikubwa na midogo huku akitoa wito kwa mashirika ya umma, watu binafsi na taasisi mbalimbali kujiunga na benki hiyo.

“Kasi yetu inachochewa zaidi na kauli mbiu ya Mh. Rais John Magufuli ya ‘hapa kazi tu’ inayoenda sambamba na kuhimiza maendeleo ya viwanda na ndio maana miongoni mwa mwa huduma tunazotoa ni pamoja na mikopo kwa ajili ya viwanda,’’ alisema.

Kwa mujibu wa Bw Nyabundege benki ya TIB Corporate kwa sasa ina wateja takribani 12,000 huku ikitarajia kuvutia zaidi makampuni na taasisi (corporate clients) kutumia benki hiyo, hatua aliyoitaja kuwa itafanikiwa kupitia uwepo wa huduma bora katika benki hiyo.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Bohari Kuu ya Dawa nchini, Bw Laurean Bwanakunu ambae taasisi yake ni mteja wa benki hiyo alisema aliipongeza benki hiyo kwa kutoa huduma bora huku akiahidi kuwashawishi mashirika mengine ya umma kujiunga na benki hiyo.

“Binafsi nafarijika sana kuona kwamba taasisi yangu ambayo ni umma inafanya kazi na taasisi ya fedha ya umma tena kwa ufanisi mkubwa ndio maana naahidi kuwashawishi wenzangu ili waje kwa wingi kuunga mkono jitiahada za serikali katika kuboresha taasisi zake za fedha,’’ alisema.

Ili kuwaongezea wigo wa kibiashara wateja wake, benki hiyo hivi karibuni iliingia mkataba wa ubia na Benki ya Posta Tanzania (TPB) unaoiwezesha benki hiyo kutoa huduma zake kupitia matawi makubwa 30 na madogo 30 ya benki ya Posta yaliyopo kote nchini.

Hivi karibuni pia benki hiyo ilifungua tawi lake kwenye ofisi za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ikilenga kusogeza huduma zake kwa ubora zaidi katika bandari hiyo.

No comments:

Post a Comment