Friday, October 7, 2016

RAIS MAGUFULI ATOA MIEZI 2 KWA TANESCO KUFIKISHA UMEME KIWANDA CHA BAKHRESA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.John Pombe Magufuli akikata utepe kuzindua kiwanda kipya cha kuchakata Matunda cha Bhakresa Food Product kilichopo Mkuranga, Pwani.Kulia kwake ni Mwenyekiti wa makampuni ya Bhakresa  Bw. Said Salim Bhakresa. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.John Pombe Magufuli akipata maelezo toka kwa Mkurugenzi wa Masuala ya Jamii wa Bahkresa Group Bw.Hussein Yusuph Ally (mwenye kofia nyeupe) jinsi matunda yanayotumika kutengeneza juisi yanavyo- hifadhiwa katika mapipa maalum. Katikati ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe.Charles Mwijage na kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Azam Media Bw.Yusuph Bhakresa akitoa neno la Ukaribisho na maelezo mafupi kwa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.John Pombe Magufuli  juu ya kiwanda kipya  cha kuchakata Matunda kilichojengwa Mwandege, Mkuranga, Pwani. Wengine Kushoto kwake ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe.Charles Mwijage, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo na Mwenyekiti wa Kampuni za Bhakresa, Bw. Said Salim Bhakresa.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo akitoa salamu za mkoa wa Pwani kwa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.John Pombe Magufuli(katikati waliokaa) kabla hajaongea na Uongozi na  wafanyakazi  wa kiwanda cha Azam leo.Wengine Pichani ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe.Charles Mwijage na Mwenyekiti wa Kampuni za Bhakresa,Bw.Said Salim Bhakresa. 
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage akizungumza na Uongozi na wafanyakazi  wa kiwanda cha Bhakresa Food Product  kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kuzungumza. Kushoto kwake ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.John Magufuli na Mwenyekiti wa Kampuni za Bhakresa, Bw. Said Salim Bhakresa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.John Magufuli akiongea na Uongozi na wafanyakazi wa kiwanda cha Bhakresa Food Product mara baada ya kuzindua kiwanda cha kuchakata Matunda kilichopo Mkuranga, Pwani. Kushoto kwake ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mh. Charles Mwijage na Mwenyekiti wa Kampuni za Bhakresa, Bw.Said Salim Bhakresa. 

Na Frank Shija, MAELEZO
TENESCO yapewa miezi miwili kuhakikisha inafikisha huduma ya umeme katika kiwanda cha kusindika matunda na kuzalisha juisi na vinywaji baridi cha Bakhresa Food Products Ltd kilichopo Mwandege wilayani Mkuranga, Mkoani  Pwani.

Agizo hilo limetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kiwanda hicho iliyofanyika leo wilayani Mkuranga, Mkoani Pwani.

Amesema kuwa ni ajabu kwa mwekezaji kuanza ujenzi hadi anamaliza na baadaye anaanza uzalishaji halafu suala la nishati ya umeme linakuwa kikwazo hali inayomlazimu mwekezaji kutumia nishati mbadala (Jenereta) kitu kinachosababisha gharama za uendeshaji kuwa kubwa.

“Ninaagiza hakikisheni mnafikisha umeme katika kiwanda hiki kabla ya mwezi wa 12, nia ajabu sana mtu anaanza kujenga mnamuangalia tu, anamaliza mnamuangalia, Meneja wa TANESCO upo? Hakikisha umeme unafika kama kuna mtu ana kukwamisha niambie”. Alisema Rais Magufuli.

Aliongeza ni imani yake kuwa baada ya umeme kufikishwa katika kiwaanda hicho gharama za undeshaji zitapungua na kupelekea kufanya maboresho ya maslahi ya wafanyakazi wake.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli ametumia wasaa huo kumuomba Mwenyekiti  wa Makampuni ya Bakhresa Said Salim Bakhresa kuangalia uwezekano wa kufanya uwekezaji kama huo katika maeneo mengine ya kikanda hili kutoa fursa kwa wananchi wanaoishi katika maeneo hayo kupata soko la bidhaa zao.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage amesema kuwa uwekezaji uliofanywa na Makampuni ya Bakhresa unasaidia kuchochea kilimo cha matunda na kutoa fursa ya soko la uhakika kwa wakulima.

Mwijage alisema kuwa Sekta ya Viwanda nchini imeendelea kukuwa, aliongeza kuwa adhima ya kufikia Tanzania yenye uchumi wa kati kutokana na viwanda itatimia endapo wafanyabiashara wenye viwanda  watakua wazalendo kama Bakhresa.

Naye Mwakilishi wa Kampuni ya Bakhresa Food Production Ltd Bw. Yusuph Bakhresa ameishukuru Serikali kwa kutoa ushirikiano kwa wafanyabiashara wenye viwanda nchini, hali ambayo itasaidia kufikia lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ya kuitaka Tanzania kuwa nchi yenye viwanda ifikapo mwaka 2025.

No comments:

Post a Comment