Thursday, October 13, 2016

SERIKALI YAANZA UTAFITI WA KUANGALIA HALI YA UPATIKANAJI WA NISHATI NCHINI


Mwakilishi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Bw. Ephraim Kwesigabo akifafanua jambo kwa waandishi wa habari juu ya utafiti watakaoufanya kwa pamoja na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ukiwa na lengo la kukusanya takwimu rasmi zinazohusu hali ya upatikanaji wa nishati ya umeme katika maeneo ya vijijini. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga.(Picha zote na Daudi Manongi, Maelezo) 
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga akizungumza na waandishi wa habari juu ya utafiti ambao Serikali itaanza kuufanya kuangalia hali ya upatikanaji wa Nishati nchini hasa maeneo ya Vijijini. Kulia ni Mwakilishi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bw. Ephraim Kwesigabo.

Na Beatrice Lyimo-Maelezo
12/10/2016
Dar es Salaam
SERIKALI imeanza utafiti wa kuangalia hali ya upatikanaji wa Nishati Tanzania  katika mikoa 26  ya Tanzania bara wa mwaka 2016 kuanzia Octoba 10, hadi Novemba 15 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mwakilishi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) Dkt. Ephraim Kwesigabo amesema kuwa utafiti huo unafanya na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini(REA) kwa kushirikiana na kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Dkt Kwesibago alisema kuwa lengo la utafiti huo ni kukusanya takwimu rasmi zinazohusu hali ya upatikanaji wa Nishati umeme katika ngazi ya jumuiya na kaya,matumizi ya umeme na nishati jadidifu pamoja na faida zake kwa maendeleo.

Sambamba na ukusunyaji wa takwimu hizo, Dkt Kwesibago alisema kuwa utafiti huo utahusisha ukusanyaji wa takwimu za kidemografia na za kiuchumi za wanakaya zikijumuisha umri, jinsia, hali za ndoa, elimu, shughuli za kiuchumi, matumizi ya muda pamoja na ushiriki wa jinsia katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Aliongeza kuwa utafiti huo utahusisha jumla ya maeneo 676 ya vijiji na mijini yaliyochaguliwa kitaalam katika mikoa yote ya Tanzania bara na kuhusisha jumla ya kaya binafsi 10,140 pamoja na viongozi wa vijiji na mitaa 676 ambao watahojiwa kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopatikana katika maeneo yao.

Aidha, alisema kuwa timu ya wadadisi wapatao 130 watahusika katika zoezi hilo la ukusanyaji taarifa ambapo kila mkoa utakuwa na wadadisi watano, msimamizi mmoja na wataalamu wengine kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu makao makuu.

Vile vile alisema kuwa upatikanaji wa takwimu hizo utasaidia katika kuandaa taarifa kuhusu hali halisi ya upatikanaji na usambazaji wa nishati ya umeme nchini na hivyo kuweza kupima na kuhakiki maendeleo yaliyofanikiwa na mafanikio ya juhudi za Serikali.

Pia  taarifa za utafiti huo zitatumika katika kuendeleza mipango ya usambazaji wa umeme vijijini kupitia miradi mbalimbali itakayotekelezwa na Serikali kwa ajili ya kuongeza wigo wa upatikanaji wa nishati bora vijijini.


Mbali na hayo wananchi wameombwa kutochukua sheria mkononi kwa kuwadguru wadadisi wanapokuwa wakifanya tafiti mbalimbali kwa ajili ya kusaidia nchi yetu kupata takwimu rasmi zinazosaidia katika kutunga sera na kupanga mipango ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment